TAIFA STARS KUPEPETANA NA MALAWI LEO

Timu ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) leo itakuwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya timu ya taifa ya Malawi, The Flames.
Huo utakuwa mchezo wa kwanza kwa kocha mpya wa timu hiyo, Mholanzi Mart Nooij aliyechukua mikoba ya Mdenishi Kim Poulsen ambaye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilisitisha mkataba wake wa kuinoa timu hiyo.
Kwenye mchezo uliopita wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Burundi ambapo Taifa Stars ilikubali kulala mabao 3-0 nyumbani, Mart Nooij alikuwa jukwaani akiangalia kikosi hicho kabla ya kuanza kibarua rasmi cha kuifundisha.
Katika mchezo huo, Stars ilichezesha wachezaji wengi chipukizi waliotokana na mkakati wa TFF kusaka vipaji kwa kushirikisha timu za madaraja ya chini na kupata chipukizi hao waliowekwa kambini Tukuyu kabla ya mechi hiyo.
Kutokana na uzoefu mdogo wa nyota hao, kocha Nooij aliamua kuwarejesha kundini mabeki Nadir Haroub, Shomari Kapombe ambaye sasa amesajili katika klabu ya Azam, John Bocco wa Azam, mshambuliaji Hussein Javu na kiungo Hassan Dilunga, wote kutoka Yanga.
Nooij  pia alimuita kwa mara ya kwanza beki wa kushoto wa Yanga, Oscar Joshua baada ya kuangalia mkanda wake wa video na kuridhishwa na uwezo wake.
Mechi ya leo dhidi ya Malawi ni muendelezo wa maandalizi ya Taifa Stars kwa ajili ya kuwania kufuzu michuano ya Mataifa Afrika itakayofanyika mwaka 2016  Morocco na kutokana na uwepo wa kocha Nooij kwenye kipigo dhidi ya Malawi, ni wazi atakuwa amejua ubora na udhaifu wa timu hiyo na hivyo kujua pa kuanzia.
Kwenye kufuzu kwa fainali hizo za Afcon, Taifa Stars imepangwa kucheza mchezo wa  mtoano dhidi ya timu ya taifa ya Zimbabwe baadae mwezi huu na hivyo kupata kibali cha kuingia hatua ya makundi ya kuwania michuano hiyo.
Malawi inayonolewa na kiungo wake wa zamani, Young Chimodzi aliyepewa jukumu hilo baada ya kocha wa zamani wa Yanga, Tom Saintfiet aliyeshindwa kuiongoza timu hiyo kwa ajili ya fainali za kombe la Dunia Septemba mwaka jana, imepangwa kucheza mchezo wake wa awali kwa ajili ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika dhidi ya Chad.
Hiyo ni mechi muhimu kwa timu zote kwa ajili ya maandalizi kuelekea mechi zao hizo ambapo kama watashinda itaziwezesha timu hizo kuingia katika hatua ya makundi ya mashindano hayo.
Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam mwaka 2012 zilitoka sare ya bila kufungana, kipindi hicho Taifa Stars ikiwa chini ya kocha Kim Poulsen na Malawi ikiwa chini ya Kinnah Phiri. Nani ataibuka na ushindi katika mchezo, dakika 90 ndizo zitaamua.

No comments: