VODACOM, CALVARY ZAUNGANISHA NGUVU YA MAWASILIANO

Kampuni za Vodacom Group Limited na Cavalry Holdings Limited zimeungana baada ya Tume ya Ushindani (FCC) kuridhia maombi ya muungano wa kampuni hizo.
Muungano wa Vodacom na Cavalry Holdings Limited iliyokuwa na asilimia 17.2 ya hisa za Vodacom Tanzania, unahusu huduma za mawasiliano ya simu baada ya Tume hiyo kuridhia bila masharti maombi ya kampuni hizo. Kwa muungano huo, sasa Vodacom Group na Cavalry zitakuwa na jumla ya hisa 82.2, kwani awali, Vodacom Tanzania ilikuwa na hisa asilimia 65.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa FCC, Frank Mdimi, tume hiyo imeridhia maombi matatu ya muungano ya kampuni kwa mujibu wa kanuni Namba 42(13) ya Kanuni za Utendaji za Tume ya Ushindani za mwaka 2013.
Alisema tume hiyo imeridhia maombi matatu ya muungano wa kampuni hizo katika kikao chake cha 55 cha mashauri ya ushindani kilichofanyika Aprili 17, 2014 baada ya maombi hayo kuwasilishwa katika Ofisi za Tume kati ya Desemba 20, 2013 na Machi 28, 2014 na kampuni zilizokuwa zikikusudia kutekeleza makubaliano ya muungano huo.
Mdimi alitaja muungano mwingine ulioridhiwa na tume hiyo ni baina ya kampuni za AVIS Southern Africa na Tanzuk Limited ambao muungano wao unahusisha biashara ya ukodishaji wa magari pamoja na huduma zinazoambatana nazo na muungano baina ya kampuni za Dutch Oak Tree Foundation na Tanga Dairies Co-operative Union na Tanga Fresh Limited ambazo muungano wao unahusisha sekta ya biashara ya maziwa.
Alisema kati ya Julai 1, 2013 na Machi 28, mwaka huu, FCC imeridhia jumla ya maombi 21 ya miungano ya kampuni iliyotolewa taarifa na kuwasilishwa kwa tathmini katika tume yakiwemo maombi ya miunganiko hiyo mitatu.

No comments: