Tuhuma 3,099 za rushwa zikiwemo mpya 679 zilichunguzwa ambapo uchunguzi wa tuhuma 666 ulikamilika katika kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014.
Aidha kiasi cha Sh bilioni 39.9 kiliokolewa baada ya
kutolewa taarifa zinazohusiana na wizi wa mali ya umma.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Umma, Celina Kombani jana
wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya matumizi ya fedha kwa mwaka 2014/ 2015.
Alisema kati ya tuhuma hizo ambazo uchunguzi
umekamilika majalada 234 yaliombewa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)
ambapo majalada 174 yalipata kibali cha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani.
Pia majalada 139 ya uchunguzi maalumu wa vocha za
pembejeo yalifanyiwa uchunguzi ambapo 19 yaliombewa kibali cha mashtaka na kati
ya hayo majalada manne yalipata kibali cha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani.
Aidha alisema majalada yanayohusu maliasili ya nchi
yalifanyiwa uchunguzi ambapo majalada 10 yaliombewa kibali cha Mkurugenzi wa
mashtaka na kati ya hayo, majalada manne yalipata kibali cha mashtaka.
Alisema majalada manne yaliyohusu tuhuma kubwa za
rushwa yalifikishwa kwa mkurugenzi wa mashtaka kuombewa kibali cha mashtaka.
“Kupitia vyanzo tofauti vya taarifa zinazohusiana na
wizi wa mali za umma kiasi cha Sh 39,910,523,898 kiliokolewa,” alisema.
Waziri Kombani alisema katika kipindi cha kuanzia
Julai 2013 hadi Machi 2014, Wizara yake
ilitoa vibali vya ajira mpya kwa watumishi wa umma 50,155 kati ya nafasi 61,915 zilizoidhinishwa katika
bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/2014 sawa na asilimia 81.
Alisema madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi
wa umma yameendelea kulipwa hadi kufikia Machi 2014 jumla ya madai ya
watumishi 56,622 yenye thamani ya Sh 55,993,095,061.95 yalipokelewa.
Pia madai ya watumishi 45,048 yenye thamani ya Sh 41,760,794,348.95 yalihakikiwa na kuingizwa kwenye mfumo tayari kwa malipo kati yao watumishi 41,952 wamelipwa malimbikizo ya mishahara
yenye thamani ya Sh 36,236,611,127.75.
Malipo ya malimbikizo ya watumishi 3,096 yenye thamani
ya Sh 5,524,183,221 yapo kwenye mfumo yakisubiri kulipwa. Madai ya malimbikizo
ya watumishi 11,574 yenye thamani ya Sh 14,234,300,713 yapo kwenye hatua ya
uhakiki kabla ya kuingizwa kwenye mfumo wa malipo.
Waziri Kombani alisema utafiti kuhusu uelewa wa
viongozi juu ya maadili ya uongozi na sheria ya maadili ya viongozi wa umma
ulifanyika na kuhusisha viongozi 540 kati ya hao viongozi 514 sawa na asilimia
95.2 walisema wanaifahamu sheria hiyo na viongozi 26 sawa na
asilimia 4.8 walisema hawaifahamu.
No comments:
Post a Comment