SHULE YA TUSIIME YANYAKUA TUZO 12 DAR ES SALAAMShule ya Msingi ya Tusiime ya Dar es Salaam imeng’ara katika tuzo zilizotolewa na Mkoa wa Dar es Salaam kwa kunyakua tuzo 12.
Tuzo hizo zimetokana na kuwa na wanafunzi kumi bora kwa upande wa wasichana na kumi bora kwa upande wa wavulana kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka jana.
Hafla hiyo ya kuzipongeza shule bora na wanafunzi bora ilifanyika juzi jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mushi.
Akizungumza kabla ya kukabidhi tuzo hizo, Mushi alisema shule na wanafunzi waliofanya vizuri wanastahili kupongezwa ili iwe chachu kwa wanafunzi wengine.
Alisema Mkoa wa Dar es Salaam umejitahidi kufikia ufaulu wa asilimia 75 ingawa haukufikia lengo la matokeo makubwa sasa hivyo aliwaomba wadau wa elimu kuongeza bidii ili kufikia malengo tarajiwa.
Alisema ufaulu kwa sekondari katika mitihani ya kidato cha nne umeshuka hadi asilimia 59 hivyo aliwaomba wadau watazame changamoto hiyo na wawe na uhakika na matarajio wanayotarajia.
Mwanafunzi bora kimkoa ni Hussein Hemed Hussein kutoka Tusiime aliyepata alama 244 kati ya 250 zilizohitajika na ndiye alikuwa mwanafunzi bora kitaifa katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana.
Akizungumza mara baada ya shule yake kutwaa tuzo hizo, Mkurugenzi wa Shule za Tusiime, Albert Katagira, alisema usimamizi mzuri na ufuatiliaji wa taaluma shuleni kwake ndiyo siri ya matokeo mazuri ya shule yake kila mwaka.
Alisema shule yake ina kitengo cha ufuatiliaji ambacho kimekuwa kikifuatilia kwa karibu mwenendo wa taaluma kwa walimu wanavyofundisha na maendeleo ya wanafunzi kitaaluma siku hadi siku, hali ambayo imekuwa ikileta chachu kwa wanafunzi kusoma kwa bidii.
Shule zingine zilizoingia kumi bora Dar es Salaam ni Montfort, St Joseph Millennium, Fountain of Joy, Hazina, Nyiwa, Heritage, Holy Cross, New Ambassador na Azanak.

No comments: