VIJIJI, MGODI WA NORTH MARA WAANZA KUELEWANA


Uhusiano wa kijamii kati ya mgodi wa North Mara na vijiji vinavyozunguka umeendelea kukua kutokana na jitihada za menejimenti ya kampuni hiyo kurekebisha kasoro zinazojikeza kati ya pande hizo mbili kwa njia rafiki.
Awali, mgodi huo ulio chini ya Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya African Barrick Gold (ABG) ulikuwa ukikabiliwa na vurugu za mara kwa mara za wavamizi wa maeneo ya uchimbaji kwa nia ya kuiba pamoja na wanavijiji waliokuwa wakidai kuwa mgodi unawahujumu.
Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa mgodi huo, Gary Chapman, licha ya kuendelea kuwepo kwa watu wanaoingia kuchambua mawe yaliyorundikwa na kuchukua madini isivyo halali, wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwadhibiti bila kusababisha uvunjifu wa amani wala chuki miongoni mwa jamii hizo mbili.
Akizungumza na gazeti hili, Chapman alisema, wanatumia mikakati rafiki kama vile kuwafadhili wavamizi wanaokuwa tayari kuacha wizi na kuanzisha miradi ya kiuchumi, kujenga ukuta katika maeneo yenye wizi wa madini uliokithiri katika mgodi huo, kutoa huduma muhimu kwa jamii inayowazunguka pamoja na kurudisha faida kwa wanajamii yenye mahitaji kwa njia wanazozipendekeza (wanavijiji).
Aidha, aliongeza kuwa pamoja na kutekelezwa kwa mikakati hiyo, kampuni imeendelea kutoa elimu kwa jamii inayouzunguka mgodi kuhusu faida za kuwepo kwa mgodi huo, faida ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili na hasara ya kuuhujumu kwa uchumi wa eneo hilo na maendeleo ya wanavijiji pia.
Alisema, “Hadi sasa wanavijiji wameanza kupata mwamko wa kushirikiana na mgodi katika masuala mbalimbali ya maendeleo kwenye maeneo yao ya makazi, badala ya kuupinga na kuuhujumu. Changamoto iliyobaki ni kwa wachache wanaoendeleza uvamizi na kuharibu miradi ya jamii tunayoidhamini.”
Baadhi ya miradi iliyotembelewa na gazeti hili ikiwa ni matunda ya ufadhili wa mgodi huo ni pamoja na shule za msingi na sekondari, nyumba za walimu, zahanati, mradi wa kupasua kokoto unaomilikiwa na wazee na miradi tofauti ya vijana walioachana na uvamizi wa mgodi huo.

No comments: