SHILINGI MILIONI 540 ZATENGWA KUKABILI HOMA YA DENGUE



Shilingi milioni 132 zimetumika, huku Sh milioni 540 zikitengwa kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa dengue, ulioibuka hivi karibuni jijini Dar es Salaam.   
Aidha, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeshafanya utafiti mkoani  Kagera, Morogoro na Kigoma na kuthibitisha kuwa  haijaathirika na ugonjwa  huo.  
Wakati ugonjwa huu umetajwa kukumba zaidi ukanda wa joto, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeandaa mpango kwa kushirikiana na sekta mbalimbali kuudhibiti.  
Taarifa hiyo ilitolewa  jana na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Stephen Kebwe  ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Kiti cha Spika baada ya Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile kuomba mwongozo wa spika juzi, kutaka Serikali kutoa taarifa rasmi bungeni.  
Dk Kebwe ambaye alisema Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kukabili ugonjwa huu kadri itakavyohitajika, alihimiza uvaaji wa nguo ndefu na zenye mikono mirefu, hususani katika maeneo ambayo ugonjwa huu umeripotiwa. 
Alisema timu ya taifa ya maafa, inayoshirikisha halmashauri za Kinondoni, Temeke na Ilala inaendelea kukutana kila wiki. 
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeshafanya utafiti katika mikoa ya Kagera, Morogoro na Kigoma na kuthibitisha kuwa haijaathirika na mkoa huo.  
Ugonjwa huo unaotokana na kirusi, kinachosambazwa na mbu aina ya Aedes, idadi ya wagonjwa tangu Januari mwaka huu hadi sasa ni 458 na vifo vitatu.  
Dalili za ugonjwa huo ni homa, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu huku wakati mwingine, dalili zake zikifanana na za malaria. 

No comments: