Ofisa
Uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Thadei
Nzalalila, ameieleza Mahakama kwamba aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Viwango
Tanzania (TBS), Charles Ekelege alikiri kutoa msamaha wa ada ya utawala kwa
kampuni mbili.
Nzalalila
alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati akitoa ushahidi
katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kulisababishia shirika hilo
hasara ya Sh milioni 68, inayomkabili Ekelege.
Ekelege
anadaiwa kusababisha hasara hiyo, baada ya kuondoa ada ya asilimia 50, ambayo
ni sawa na Sh milioni 68 kwa kampuni za Jaffar Mohamed Ali na Quality Motors
bila idhini ya Bodi.
Akiongozwa
na Wakili kutoka Takukuru, Janeth Machulya, Nzalalila alidai kuwa alimhoji
Ekelege na katika maelezo yake ya onyo, alikiri kusamehe kodi kampuni hizo na
alitoa msamaha wa dola 27.380 kwa Kampuni ya Jaffar Mohamed Ali na dola 15.160
kwa Kampuni ya Quality Motors.
Alidai
katika maelezo yake kuwa Ekelege alifanya hivyo kwa kuwa aliamini kampuni hizo,
zipo chini ya kiwango, ambacho anaruhusiwa kufanya hivyo kisheria.
Awali
alidai kuwa mwaka 2012 na 2013, alifanya uchunguzi kuhusu tuhuma dhidi ya
Ekelege, na kugundua ni kweli kampuni hizo ziliandika barua za kuomba msamaha
wa kodi, ambapo Ekelege alifanya hivyo, bila kushirikisha Idara ya Fedha na
utawala ya shirika hilo.
Aidha,
alidai hakukuwa na kikao chochote kilichofanywa na menejimenti kupitisha
msamaha huo, pia ripoti ya ukaguzi wa ndani ya TBS, ilijadiliwa na Bodi ya
Wakurugenzi ambayo iliidhinisha msamaha huo ambao tayari ulikuwa umeshatolewa.
Inadaiwa
kuwa Machi 28, mwaka 2008 na Agosti 7, mwaka 2009, Ekelege alitumia madaraka
vibaya kusamehe ada kampuni mbili kwa asilimia 50, ambayo ni sawa na Sh milioni
68 bila idhini ya Baraza la Utendaji, kinyume na utaratibu wa TBS na pia
alilisababishia shirika hilo hasara ya fedha hizo.
No comments:
Post a Comment