WAFANYAKAZI TAZARA WAGOMA WAKIDAI KULIPWA MISHAHARA YAOWafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) wamegoma kufanya kazi kwa  kushinikiza kulipwa mishahara yao ya miezi mitatu.
Wafanyakazi hao walianza mgomo huo juzi wakishinikiza uongozi wa mamlaka hiyo kuwalipa mishahara yao ya kuanzia mwezi Februari mpaka Aprili, mwaka huu na pia madai ya mamlaka hiyo kuzembea katika usimamizi wa vitendea kazi.
Jana safari za kwenda Kapili Mposhi nchini Zambia na kuja Dar es Salaam zilifutwa kutokana na mgomo huo ambao pia umehusisha treni inayofanya safari zake kutoka kituo cha Tazara mpaka Mwakanga.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyanyakazi wa Reli nchini (Trawu), Dar es Salaam yasin Mleke alisema, wafanyakazi wamekuwa wakifanya kazi bila malipo yao hali inayowafanya kuishi katika hali ngumu.
"Wafanyakazi wamekuwa na njaa tangu Februari. Wananusirika kwa kukopa chakula katika maduka mbalimbali na baadhi yao tayari wameshaenda kushitakiwa katika ofisi za serikali za mitaa kujibu mashtaka kwa kutolipa madeni," alisema Mleke.
Aidha, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Tazara, Conrad Simuchile alinakunusha madai ya kuwepo kwa uzembe na kusema, "Katika miezi 12 iliyopita Tazara kwa wastani ilikpata mapato ya karibu dola za Marekani milioni 2.5.
"Kati ya kiasi hicho, angalau dola za Marekani milioni 1.4 huenda kwa wafanyakazi kwa ajili ya  mishahara ya kila mwezi, mafuta ya kuendesha injini, matengenezo ya madaraja na mahitaji mengine, " alisema Simuchile.
Alisema katika kipindi cha mwezi Januari na Machi tani 4,000 za mizigo zilizafirishwa kwa wastani kwa mwezi na kuzalisha kiasi cha dola za Marekani 400,000, kiasi ambacho hakitoshi hata kulipa theluthi moja ya wafanyakazi hao.
Katibu wa Trawu tawi la Dar es Salaam Waziri Mwenevyale aliishauri menejimenti ya Tazara kuacha ubaguzi linapokuja suala la usafirishaji wa mizigo..
Alisema ni wakati wa Tazara kushiriki katika biashara kubwa na kuachana na siasa zisizo na manufaa. "Ni ajabu kwamba hata baadhi ya maamuzi eti yanatolewa na mikoa, utawala ni kama umetekwa nyara na Makao Makuu na kama mikataba inavyoelekeza katika sheria ya Tazara ya mwaka 1995," alisema.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa abiria aliyekuwa akisafiri kuelekea Mbeya aliyejitambulisha kwa jina la Amina Said alisema kuwa mgomo huo kwa kiasi kikubwa umewagharimu kutokana na wengi wao kutoka mbali na wana watoto wadogo.
"Hata wewe huyu mtoto mdogo niliyenaye hapa anapata tabu kwa sababu kwanza baridi, kwa hiyo tunaomba tuangaliziwe namba nyingine ya kusaidiwa kuweza kufika tunapoenda na hasa kwa kuangalia tunatoka mikoani," alisema.

No comments: