SHERIA YA KAMATI YA BUNGE YA BAJETI YAJASpika wa Bunge, Anne Makinda amesema Bunge la Tanzania liko katika mchakato wa kuandaa Sheria na Kanuni itakayosimamia idara mpya, inayotarajiwa kuundwa itakayosimamia na kuongoza shughuli zote za Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Makinda alisema hatua hiyo, inatokana na Bunge hilo kutambua changamoto iliyopo ndani ya kamati hiyo, ambayo ni pamoja na ukosefu wa idara hiyo nyeti ya kuisimamia.
Alikuwa akifungua semina ya siku tano ya 25 ya Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA), inayofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo Tanzania ni mara yake ya kwanza kuwa mwenyeji wa semina hiyo.
“Katika dunia ya leo ya utandawazi, mabunge mengi duniani yako katika mchakato wa mageuzi katika utendaji wake ili kuhakikisha shughuli na uwajibikaji wake unawafikia ipasavyo na kwa uwazi wananchi, na Bunge la Tanzania ni moja ya mabunge hayo yanayopitia mageuzi hayo,” alisema Makinda.
Alisema katika Bunge la 10, Bunge hilo, lilipitia mageuzi kadhaa kwa ajili ya kuliimarisha ikiwemo kuanzishwa kwa kamati hiyo ya bajeti ambayo imetimiza takribani mwaka mmoja sasa tangu kuanzishwa kwake.
Alisema katika kipindi hicho, kamati hiyo imeweza kuimarisha ushiriki wa Bunge la Tanzania katika mchakato mzima wa uandaaji wa bajeti ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Bunge hilo, limeweza kubadili baadhi ya vifungu vya fedha na kupendekeza maeneo yenye umuhimu kwa wananchi kupewa kipaumbele.
Akizungumzia mada itakayowasilishwa na kujadiliwa katika semina hiyo inayohusu mbunge anawajibika kwa nani, chama, Bunge au taifa lake? Makinda alisema mada hiyo ni muhimu kwa kuwa itatoa dira na mafunzo kwa wabunge ikiwa ni pamoja na kutoa mwanga juu ya hatua zitakazochukuliwa kwa mbunge asiyetambua wajibu wake.
“Mada hii itatoa mwanga na kuwapa uelewa wabunge wa kujitambua, kwa kuwa hili ni tatizo hata hapa nchini, kuna kesi mbalimbali zinaendelea katika mahakama za nchi wanachama wa CPA ikiwemo sisi Tanzania tuna kesi mbili za wabunge juu ya tatizo hili,” alisema Makinda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CPA Tawi la Tanzania, Mussa Zungu, alisema semina hiyo pamoja na mambo mengi inatoa changamoto kwa wabunge kufuata kanuni ndani ya Bunge na kutambua wajibu wao.
Akitolea mfano, suala la baadhi ya wabunge waliounda chama cha Umoja wa Katiba ya Watanzania (UKAWA), alisema wabunge hao wanatakiwa kutumia busara na kurejea bungeni baada ya kuzunguka kwa wananchi, kwa kuwa ndani ya Bunge ndipo hoja zao zitakapofanyiwa kazi.
Katibu Mkuu wa CPA, Dk William Shija, alimkabidhi Spika Makinda
kitabu kinachoitwa ‘Following the Money’ ambacho kinazungumzia kanuni za Bunge katika kusimamia na kufuatilia matumizi ya Serikali.
Semina hiyo imejumuisha wabunge 60 kutoka nchi 18 wanachama wa CPA, wakiwemo wageni maarufu kama vile Spika wa Bunge la Uganda, Rebecca Kadaga, Naibu Spika wa Bunge la Malasyia Ronald Kiandee, Spika wa Jimbo la Australia Mashariki Barry House na Mnadhimu Mkuu wa Serikali ya Ghana, Dk Benjamin Bewa-Nyogo Kunbour.

No comments: