WAANDISHI WAHIMIZWA KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALIISerikali imetaka vyombo vya habari, kutumia ushawishi wake kwa jamii, kuripoti shughuli za utalii na kuvitangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini kuhamasisha utalii wa ndani na nje.
Hayo yalielezwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi wakati akifungua warsha ya wahariri wa vyombo vya habari, inayofanyika jijini hapa.
“Ni wakati muafaka sasa kwa vyombo vya habari kuamua kwa makusudi na kwa kuongeza uhamasishaji kwa jamii kwa kuvitangaza ili jamii iweze kuvitembelea,” alisema.
Alisema vivutio vya utalii, vipo katika maeneo yote nchini na kwamba utalii unapaswa kuwa endelevu na usiyumbe, utalii wa ndani unahitajika  hivyo kasi ya uelewa, inahitajika kwa vyombo vya habari kujulisha umma.
Tarishi alisema utalii ni moja ya sekta,  ambazo huchangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa Tanzania, ambapo kwa mwaka jana inakadiriwa uliingiza dola za Marekani bilioni 1.8.
Aidha, alisema tafiti zinaonesha sekta ya utalii, ilitoa  ajira 1,196,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Alisema katika mwaka huo, Tanzania ilipokea watalii wa nje wapatao 1,135,884. Alitaka vyombo vya habari kutumika katika kutangaza vyema vivutio na hifadhi ili ziweze kutembelewa na wageni wengi zaidi.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Ibrahimu Musa alisema eneo la utalii wa ndani ni changamoto kubwa kwa shirika, licha ya sekta ya utalii kutoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi.
Alisema mkutano huo, ambao unafanyika kwa mara ya pili  na kuwahusisha wahariri wa habari,  una kaulimbiu inayosema ‘Wajibu wa Vyombo vya Habari katika Kukuza Utalii’.
Warsha hiyo imeandaliwa na Tanapa, yenye dhamana ya kusimamia maeneo yote, yaliyotengwa kisheria kama hifadhi.

No comments: