SERIKALI YATAKIWA KUNUNUA TRENI ZA KISASA



Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imesisitiza kuwa ili mradi wa treni ya kusafirisha abiria jijini Dar es Salaam, ufanyike kwa kasi na kwa ufanisi, Serikali iharakishe kununua angalau treni mbili za kisasa.
Aidha, imeishauri kuongeza kasi katika kutafuta kampuni tanzu mahsusi kwa usafiri huo, ambayo itatoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki kutoa huduma jijini.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Serukamba alisema hayo jana bungeni wakati akitoa taarifa ya Kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi ya mwaka 2013/14 na maoni kuhusu bajeti ya 2014/15.
“Kamati inasisitiza kuwa ili mradi uweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuondokana na hasara, Serikali iharakishe kununua angalau treni mbili za kisasa na maalumu kwa safari fupi ambazo gharama yake ni takribani shilingi bilioni nane kila moja.
 “Vile vile Kamati inashauri Serikali kuongeza kasi katika kutafuta kampuni tanzu mahsusi kwa usafiri wa treni ya abiria, ambayo itatoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki katika kutoa huduma ya usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam na miji mingine nchini,” alisema Serukamba.
Kuhusu usafiri wa reli kwa ujumla, Kamati hiyo iliishauri Serikali kuchukua hatua mahsusi za kukarabati na kuimarisha mtandao wa reli nchini, hata kwa kutafuta fedha nje ya utaratibu wa kawaida wa bajeti.
Ilishauri Serikali kutoa fedha za miradi ya reli zipatazo Sh bilioni 9.8, zilizobaki katika mwaka wa fedha 2013/14 ili mabehewa yanayotengenezwa nje ya nchi, yaweza kuwasili na kuboresha huduma za usafiri wa reli nchini.
Akizungumzia viwanja vya ndege, Serukamba alisema kumekuwa na changamoto na migogoro mingi ya ardhi baina ya wananchi wanaoishi kando ya viwanja vya ndege.
“Kamati inaishauri Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi pamoja na mamlaka zingine zinazohusika na ardhi kuhakikisha inaweka mipaka katika maeneo ya viwanja vyote vya ndege na kuvipa Hati Miliki,” alisema Serukamba na kuongeza:
“Vile vile kwa maeneo ambayo yametwaliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kama vile Omukajunguti-Bukoba, malipo ya fidia kwa wananchi yafanyike haraka.”
Kuhusu Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Serukamba alihoji kama Serikali inatambua umuhimu wa kampuni hiyo na kama bado inaihitaji, na kama inaihitaji, kwa nini haitoi mtaji wa kutosha.
“Kamati inaishauri Serikali iamue kuwekeza mtaji wa kutosha ili iweze kulipa madeni yote ya ATCL hatimaye kufufua upya kampuni hii,” alisema mbunge huyo wa Kigoma Mjini (CCM).
Kwa upande wake, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Moses Machali alisisitiza Serikali kuweka mkazo katika sekta zote zinazozalisha mali na huduma muhimu kama vile usafiri wa anga, barabara, maji, elimu na afya.
“Wanasiasa wenzangu tujenge nchi yetu, tuamue sasa kwamba tuanze na kuhamisha mafungu ya fedha za matumizi yasiyo ya lazima na kuzipeleka kwenye reli na bandari mwaka huu na tuanze na hizo za Uchukuzi zenyewe,” alisema mbunge huyo wa Kasulu Mjini (NCCR-Mgeuzi).

No comments: