SERIKALI KUANZISHA BODI YA KITAALAMU YA WALIMUSerikali imeamua kuanzisha bodi ya kitaalamu ya walimu Tanzania katika mwaka ujao wa fedha, itakayosimamia masuala ya walimu, ikiwemo usajili, uendelezaji wa walimu na maadili ya kazi ya ualimu. 
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka 2014/2015. 
Alisema Wizara itaendelea kujadiliana na wadau wengine ikiwemo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuhusu suala namna bora ya kumhudumia mwalimu katika mazingira ya sasa ya ugatuaji wa huduma mbalimbali kwenda Tamisemi.  
Wakati huo huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii katika taarifa yake imetaka posho ya mazingira magumu, itolewe kwa walimu.  
Kamati hiyo imetaka Serikali kukamilisha mapema iwezekanavyo mchakato wa kutoa posho ya mazingira magumu kwa walimu, wanaofanya kazi hasa vijijini na kusisitiza umuhimu wa mafunzo kwa walimu kazini.  
Suala lingine ambalo kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Margaret Sitta inapendekeza ni Serikali kuangalia upya mfumo wa kuhudumia walimu kwa kuanzisha Tume ya Utumishi wa Walimu ili kukabili adha zinazowakabili watumishi hao.  
Wizara imeomba kuidhinishiwa Sh bilioni 799, ambazo kati yake Sh bilioni 344.2 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh bilioni  454.8 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa mwaka 2014/2015.  
Bajeti ya wizara hiyo imeongezeka kutoka Sh bilioni 689.7 mwaka 2013/2014 hadi Sh bilioni 799 mwaka 2014/2015. Pia bajeti ya matumizi ya maendeleo, imeongezeka kutoka Sh bilioni  72 mwaka huu wa fedha hadi Sh bilioni 454 kwa mwaka ujao wa fedha.  
Wakati huo huo leo ni zamu ya Wizara ya Viwanda na Biashara kuwasilisha bajeti yake bungeni. Pia Wizara ya Ujenzi itasoma bajeti yake leo, kabla ya kujadiliwa keshokutwa. 

No comments: