NEMC KUENDELEA KUWAKAMATA WANAOCHIMBA MCHANGABaraza la Taifa na Hifadhi la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), litaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wachafuzi wa mazingira, wakiwemo wanaochimba mchanga katika maeneo yasiyo rasmi.
Mwanasheria wa Baraza hilo, Manchare Suguta, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa shughuli za baraza hilo katika kusimamia mazingira.
Suguta alisema kuwa baadhi ya maeneo, yamegeuzwa kuwa machimbo ya mchanga wakati Serikali haijatenga maeneo hayo kwa shughuli hizo za uchimbaji.
"Kwa mfano yale machimbo yaliyoko maeneo ya  Mbezi tumeshawasiliana na OCD wa Kawe (Mkuu wa Polisi) ili tuanze   kuwakamata kwa kuwa wanakiuka sheria," alisema Suguta.
Alisema tangu kuanza kwa baraza hilo limechukua hatua mbalimbali za kusimamia sheria ikiwa ni pamoja na kuzuia uchimbaji holela wa mchanga katika maeneo yasiyo rasmi ikiwemo mito.
"Mfano mzuri ni kuyakamata na kuyatoza faini jumla ya malori 76 yaliyokuwa yanachimba mchanga maeneo mbalimbali yasiyoruhusiwa, lakini pia wamiliki wa malori hayo walitakiwa kurejesha mazingira ya maeneo hayo katika hali yake ya awali zoezi ambalo limeshafanyika," alisema.
Hata hivyo, alisema kuna changamoto kubwa ya uelewa mdogo wa jamii, kuhusu sheria ya usimamizi wa mazingira, ambapo wamekuwa wakishindwa kutambua kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuishi katika mazingira safi na salama.
Aidha, alisema kumekuwepo na mkinzano wa sheria za kisekta na ya mazingira, hivyo kusababisha shughuli katika maeneo ya vyanzo vya maji kufanyika, ambapo inakinzana na sheria ya mazingira.
Mkurugenzi wa Idara ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira wa NEMC, Ignance Mchallo, aliwataka wananchi kuhakikisha wanatoa taarifa za maendeleo zinazofanyika katika maeneo yao kupitia mradi wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM).
"Wananchi wanaweza kuhoji kuhusu vibali mbalimbali ikiwemo cha TAM  kupitia uongozi husika  na wawekezaji wanapaswa kuandikisha miradi au shughuli zao  za maendeleo ili zipitie mchakato wa TAM," alisema.

No comments: