PADRI AONYA WANAOSAKA UTAJIRI KUPITIA DAWA ZA KULEVYA



Katibu Mkuu wa Jimbo la Kanisa Katoliki Same, Padre Bruno Chelagwa amehadharisha vijana kujiepusha na vishawishi vya kutaka utajiri wa harakaharaka kwa kujitumbukiza kwenye biashara ya dawa za kulevya.
Padre Chelagwa alitoa tahadhari hiyo, alipokuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya tatu ya kidato cha sita katika shule ya Sekondari ya Wasichana ya Sayansi Kandoto Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro  mwishoni mwa wiki.
‘’Msidanganywe kukimbilia utajiri wa harakaharaka kwa kujitumbukiza kwenye madawa ya kulevya. Someni zaidi mpate ujuzi na kazi itakayowawezesha kuishi maisha mazuri,’’ alisisitiza.
Alifafanua kwamba elimu peke yake, haitoshi katika maisha, bali pia wanatakiwa kuzingatia utu na ubinadamu na kuongeza kuwa elimu bila utu ni kazi bure.
Ofisa Elimu wa Wilaya ya Same, Happiness Laiza aliwataka wahitimu hao, kuwa makini wanapojiunga na vyuo vya elimu ya juu kwa kujichunga na kujiongoza wenyewe.
‘’Mnapokwenda vyuo vikuu hakuna kengele ya kukuamsha, sare za shule wala geti bali ni wewe mwenyewe kujiongoza tafauti na mlivyokuwa katika ngazi ya sekondari,’’ alisema.
Aliwaasa pia kuwa makini na gonjwa hatari la Ukimwi kwa kuepuka vitendo vya ngono zembe katika maisha yao ya elimu ya juu, wanayotegemea kujiunga siku za usoni.
Ofisa Elimu huyo pia alikabidhi shule hiyo tuzo, waliyotunukiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika Wiki ya Elimu ilifanyika mjini Dodoma hivi karibuni kwa kupata matokeo mazuri ya kidato cha nne kwa mwaka 2013 kwa kushika nafasi ya 22 kitaifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo , Padre Peter Mziray,  awali katika hotuba yake kwenye mahafali hayo, aliwakumbusha wahitimu kuwa makini katika masomo yao ya elimu ya juu kwa kutobweteka kwamba wametoka kwenye shule nzuri.
‘’ Ni rahisi kwa mtu mzima wa afya kuwa mlemavu wa viungo lakini siyo rahisi kwa mlemavu wa viungo kuwa na afya njema,’’ alionya.
Katika hotuba yao, wahitimu nao pamoja na kushukuru uongozi wa shule hiyo kwa kuwapatia malezi na elimu bora, walitoa changamoto kwa shule hiyo kuongeza idadi ya walimu na vitabu kwenye maktaba ya shule.
Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Sayansi Kandoto, ina jumla ya wanafunzi 586 wa kidato cha kwanza hadi cha sita. Ni wanafunzi 11 wa michepuo ya masomo ya PCB na PCM ndiyo waliohitimu masomo yao ya kidato cha sita mwaka huu shuleni hapo.

No comments: