RAIS KIKWETE ATAKA SEKTA BINAFSI KUKABILI UKIMWI

Rais Jakaya Kikwete ameitaka sekta binafsi kujihusisha zaidi katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, kwa sababu ugonjwa huo unaathiri uchumi, biashara na kuongeza mzigo wa gharama za uzalishaji kwa kampuni.
Aidha, Rais Kikwete amesema pamoja na kwamba Tanzania imekuwa inapata michango mikubwa kupambana na Ukimwi kutoka kwa washirika wake wa maendeleo, bado jukumu la msingi la kupambana na ugonjwa huo nchini ni la Watanzania wenyewe.
Pia, Rais Kikwete aliwakumbusha Watanzania kuwa Ukimwi hauna tiba ya kisayansi ama tiba mbadala ya waganga wa jadi ama wapiga ramli kama baadhi ya Watanzania wanapenda kujiaminisha.
Rais Kikwete alizungumza usiku wa kuamkia jana katika hafla ya uzinduzi wa uchagishaji fedha za kupanda Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya mapambano ya Ukimwi kwa mwaka huu wa 2014 kwenye Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro, Dar es Salaam.
Alisema wajibu wa msingi wa kupambana na Ukimwi nchini ni wa Watanzania na hivyo Watanzania hawana budi kuendeleza mapambano hayo hata pasipo na ufadhili.
“Wajibu wa msingi wa kusimamia mapambano dhidi ya Ukimwi na kwa kuwahudumia wale walioathirika ni jukumu letu sisi Watanzania wenyewe. Hivyo, hatuna budi kuendeleza mapambano hata pale pasipo na ufadhili. Njia pekee ni kuongeza jitihada za ndani kwa kuunganisha nguvu zetu kwenye utafutaji wa rasilimali fedha.”
Uchangishaji huo chini ya Kili Challenge 2014 huendeshwa kwa pamoja na Kampuni ya Anglo Gold Ashanti kupitia kampuni tanzu yake ya uchimbaji dhahabu ya Geita Gold Mine (GGM) ya Mkoa wa Geita na mwaka huu ni mara ya 12 tokea kuanzishwa uchangishaji wa fedha za kuunga mkono mapambano ya Ukimwi.
Kiasi cha Sh bilioni 12 zimechangwa katika miaka hiyo 12 na kiasi cha makampuni 30 yaliyokuwa ya kiserikali na yanayojihusisha na mapambano dhidi ya Ukimwi yamenufaika. Aidha, katika miaka hiyo 12 kiasi cha watu 500 wameshiriki kupanda Mlima Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhamasisha mapambano dhidi ya Ukimwi.
Mwaka huu, kiasi cha Sh bilioni 2.5 zinatarajiwa kukusanywa na hadi jana kiasi cha wachangiaji 50 walikwishajiandikisha.

No comments: