FAMILIA YA MAREHEMU YAHAMAKI MTUHUMIWA KUTOSHITAKIWA

Familia ya marehemu Chacha Silas (59), mkazi wa kitongoji cha Bumangi, kijiji cha Wegero, wilaya ya Butiama, mkoani Mara, wamelalamikia kitendo cha jeshi la polisi wilayani humo, kutomfikisha mahakamani mtuhumiwa wa mauaji ya ndugu yao kwa kutumia rungu, wakiwa kwa mwanamke waliyekuwa wanamchukua kimapenzi wote wawili.
Wakizungumza na mwandishi wanafamilia hao wakiongozwa na mdogo wa marehemu Burwe Silasi Magesa, walisema kuwa ndugu yao aliuawa na Boniphace Wankuru Magabe, mkazi wa kijiji hicho kwa kumpiga na rungu kichwani.
Walisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 6, mwaka huu majira ya usiku, katika kijiji cha Wegero wilayani Butiama, mkoani hapa.
Walisema kuwa siku ya tukio ndugu yao alikwenda kwa mpenzi wake  na kwamba baada ya kufika nyumbani hapo alikuta ndani ya nyumba hiyo kukiwa na mwanamume mwingine wakifanya mapenzi na mwanamke huyo.
Walisema kuwa baada ya mwanamke huyo kufungua mlango ndipo Magabe aliyekuwa ndani ya nyumba hiyo alipompiga na rungu kichwani na kuanguka chini na kupoteza fahamu, ambapo Februari 8 mwaka huu ndugu yao alifariki dunia akipata matibabu hospitali ya mkoa wa Mara.
Waliongeza kuwa mtuhumiwa huyo alitoroka baada ya kufanya tukio hilo na kwamba alikamatwa Machi 31,  na kupelekwa katika kituo cha
polisi Kyagata, lakini Aprili 23 aliachiwa huru katika mazingira ya kutatanisha akiwa katika kituo kikuu cha wilaya ya Butiama.
Waliongeza kuwa baada ya kuachiwa huru alifika kijijini hapo na kuanza kutamba kwamba hawezi kufungwa kwani pesa zake zinafanya kazi.
Aidha, waliongeza kuwa walikwenda kulalamika polisi kuhusu mtuhumiwa huyo kuachiwa huru katika mazingira hayo bila kufikishwa mahakamani, ikiwa ni pamoja na kuwatishia kuwa atawafungulia kesi ya kashfa ili wamlipe kiasi cha Sh milioni 100.
Walisema kuwa baada ya kulalamika polisi, Aprili 28 mwaka huu, mtuhumiwa huyo  alikamatwa tena na kupelekwa polisi Butiama, ambako hadi sasa anashikiliwa bila kufikishwa mahakamani.
"Sisi kama wanafamilia kwa kweli tunasikitika na kitendo cha polisi katika wilaya ya Butiama kutomfikisha mahakamani mtuhumiwa wa mauaji kwa siku zote hizo, mara ya kwanza walimwachia katika mazingira ya kutatanisha, lakini tulipolalamika walimkamata tena sasa ni kwa nini wasimpeleke mahakamani," alihoji Magesa ambaye ni mdogo wa marehemu.
Kamanda wa polisi mkoani Mara, Kamishina msaidizi mwandamizi wa Polisi, Ferdinand Mtui, amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kuongeza kuwa bado wanafanya taratibu za kisheria ili mtuhumiwa huyo aweze kufikishwa mahakamani.
Mtui alisema kuwa hata hivyo ndugu wa marehemu walishafikisha suala hilo hata kwa mwanasheria mkuu wa serikali, hatua aliyosema kuwa hawakustahili kwenda hadi huko wakati suala hilo bado linashughulikiwa kisheria na polisi.
Aidha, aliwataka wanafamilia hao kutoa ushirikianao wa kutosha kwa jeshi hilo, ili kukamilisha upelelezi mapema katika kesi hiyo ya mauaji namba 136 ya mwaka huu, ili mtuhumiwa aweze kufikishwa mahakamani.

No comments: