POLISI YAPANGA KUNUNUA MAGARI MAPYA 700Serikali inatarajia kununua magari mapya 700 kwa ajili ya polisi ambayo yatatumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani.
Hatua hiyo inatokana na Serikali kujipanga kudhibiti uhalifu kwa kuhakikisha polisi wanakuwa na vifaa vya kisasa vitakavyowasaidia kupambana na uhalifu.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo cha kujadili bajeti iliyopita ya mwaka 2013/2014 na inayokuja ya 2014/2015.
Alisema kuwa Wizara yake inatarajia kutumia Sh bilioni 955.9 ambazo kati ya hizo Sh bilioni 691.5 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh bilioni 264.3 zikiwa ni za maendeleo.
"Idara ya Polisi ina uwezo wa kukusanya fedha nyingi na kwa mwaka huu imekusanya zaidi ya asilimia 120 kwa miezi mitatu tu," alisema Waziri Chikawe.
Alisema magari hayo yatakuwa kwa ajili ya matumizi ya polisi kwa shughuli zao zote ikiwemo kupambana na biashara haramu za dawa za kulevya, uchaguzi pamoja na operesheni nyingine watakazokuwa wakifanya kwa ajili ya kuleta hali ya usalama.

No comments: