Mbunge
wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) amesema haiingii akilini kuona Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika kuendelea kuwa madarakani licha ya kushindwa kusimamia
maeneo muhimu ya kilimo kama wakulima kupelekewa mbegu na mbolea bandia.
Alitoa
kauli hiyo jana wakati akichangia hotuba ya makadirio ya matumizi ya fedha ya
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
Alisema
wakulima wamekuwa wakipelekewa pembejeo feki na Waziri amekuwa kimya.
“Inakuwaje
Waziri, wakulima wanapelekewa pembejeo feki bado Waziri, analipa ruzuku mbegu
ya pamba isiyoota haiingii akilini,” alisema.
Alisema
kuna raia wa China ambaye alikuwa mkandarasi katika daraja huko Kilombero na
aliamua kujiua kwa ajili ya kujenga daraja lililokuwa chini ya kiwango.
Alisema
hamshauri Waziri ajiue, lakini kwa vitendo hivyo Waziri angeacha
kazi na kupumzika na kufanya kazi mbadala.
“Wizara
hii itakigharimu Chama Cha Mapinduzi (CCM) ukiangalia hotuba ya Waziri Mkuu
mwaka jana ilisema Serikali iko kwenye mchakato wa kuanzisha bima ya bei
ya pamba lakini kwenye hotuba ya Waziri hakuna mahali ambapo mfuko huo
ulizungumziwa,” alisema na kuongeza.
“Nchi
hii itaendeshwa kwa usanii mpaka lini? Itakuwaje Mbunge wa Mwibara nikuunge
mkono kwenye jambo la kisanii kama hili? Kwenye jimbo langu tuna mabonde mazuri
lakini mpaka leo tunataka tupewe skimu ya umwagiliaji, lakini Serikali ya CCM
haitaki kutusikia katika mazingira ya kudanganyana, wananchi wa Mwibara Mbunge
wao ni mimi nitakuwa mgeni wa nani? Alihoji mbunge huyo.
Alisema
hawezi kukubaliana na hotuba kila wakati maneno ni yale yale na
utekelezaji wake umekuwa ni mdogo. “Nitawaambia nini wakulima wa Mwibara?”
Akahoji.
Mbunge
wa Sumve, Richard Ndasa (CCM) alisema Waziri alikuwa wa kwanza kupinga
mbolea ya minjingu baada ya kuingia jikoni je hiyo mbolea ya minjingu inafaa?
Hata
hivyo Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde alisema mwaka jana bajeti
ya kilimo ilitengewa bilioni 81 lakini iliyotoka ni bilioni 41 hali ambayo
ilifanya baadhi ya miradi kushindwa kutekelezwa.
Mbunge
wa Viti Maalum, Esther Bulaya (CCM) alisema si sera ya CCM kufumbia macho watu
wanaofanya ubadhirifu kwenye sekta ya kilimo na kutaka kuchukuliwa kwa hatua
kwa wote wanaohujumu miradi ya kilimo.
Mbunge
wa Namtumbo, Vita Kawawa (CCM) alitaka Serikali kulipa fidia kwa wakulima
waliopata hasara kutokana na kuuziwa mbegu feki kwani wakulima wengi ni
masikini.
Huku
Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (CCM), alimtaka Waziri Mkuu na Waziri
wa Kilimo kutembelea wakulima wa pamba ili kuona changamoto wanazokabiliana
nazo.
No comments:
Post a Comment