SERIKALI YATOA UFAFANUZI KUHUSU WAKURUGENZI MALIASILISerikali imesema Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa na Mkurugenzi Msaidizi wa  Idara ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Profesa Jafari Kideghesho, hawajawahi kufukuzwa kazi ama kuadhibiwa. 
Ilisema hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, iliyotolewa na Idara ya Habari (Maelezo), Dar es Salaam jana.
Taarifa hiyo ilisema:“Kumekuwa na taarifa kwenye baadhi ya vyombo vya habari, kwamba wakurugenzi hao walikuwa wamefukuzwa kazi na Waziri wa Maliasili na Utalii, na kisha kurejeshwa kwa maelekezo ya Ikulu. Taarifa hizo si sahihi”. 
“Hata hivyo, kutokana na yaliyokwisha kutokea, wanataaluma hawa, Profesa Alexander Songorwa na Profesa Jafari Kideghesho, kwa hiari yao wenyewe, wamekubali kuchukua majukumu mengine katika utumishi wa umma kama watakavyopangiwa,” ilieleza taarifa hiyo ya Maelezo.
Profesa Songorwa amehamishiwa katika Chuo cha Wanyamapori Mweka mkoani Kilimanjaro kuwa Naibu Mkuu wa Chuo hicho, wakati Profesa Kideghesho amehamishiwa Hifadhi ya Taifa ya Selous, ambako atakuwa Meneja Msaidizi wa Mradi.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kwa mujibu wa sheria za nchi, kila mtumishi wa umma, anayo mamlaka yake ya ajira na mamlaka yake ya nidhamu ;na kwamba Mamlaka ya Nidhamu ya Profesa Songorwa na Profesa Kideghesho, haijawahi  kuwachukulia hatua zozote za kinidhamu. Lakini, baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii kuonyesha kutoridhika na utendaji wao, Mamlaka yao ya Nidhamu iliwaruhusu kuchukua likizo zao za mwaka za kawaida. Likizo zao zilipoisha, walirejea kazini kama kawaida. 

No comments: