PINDA AKANUSHA KUPISHANA NA WAZIRI MAGUFULI

Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema hakupishana maneno na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, wala kuruhusu malori yenye uzito mkubwa kupita katika mizani bila utaratibu.
Waziri Mkuu Pinda alisema hayo bungeni jana wakati akijibu maswali ya wabunge katika Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (CUF), kuhusu kuharibika kwa barabara kutokana na magari kuzidisha uzito, Waziri Mkuu alisema hakueleweka alipoingilia kati suala la Dk Magufuli kuhusu malori kuzidisha uzito.
“Bahati mbaya hili halikueleweka, na watu wakasema Waziri Mkuu ameruhusu malori kuzidisha uzito wa tani 56. Wengine wakasema tumepishana maneno na Waziri Magufuli. Hatukupishana,” alisema Pinda.
Alisema aliamua kuingilia kati suala hilo wakati wasafirishaji walipogoma, kwa sababu lilikuwa na athari kubwa kiuchumi na hasa kwa kuwa Tanzania, zaidi ya asilimia 80 ya mizigo yake inategemea usafirishaji kwa njia ya barabara.
Alisema tatizo kubwa ni kuwa usafiri wa reli haujawa nzuri na kwamba ana imani chini ya Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, reli ikitengamaa, mizigo mingi itasafirishwa kwa njia hiyo na kuzinusuru barabara.
Akimjibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (Chadema), kuhusu mabadiliko ya sheria kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, alivishauri vyama vya siasa kupeleka kwa Serikali maoni yao ili kuona namna bora ya kuyafanyia kazi kuelekea uchaguzi wa baadaye mwaka huu.
“Hata kama kukiwa na Kanuni nzuri, lakini kama dhamira yetu si nzuri, matatizo yatakuwapo. Ni lazima tufahamu sisi sote, Chama Cha Mapinduzi, upande wa Upinzani, kuwa hili ni jambo letu sote.
Pale pasipostahili pasiwe na vurugu,” alisema Waziri Mkuu. Kuhusu migogoro ya ardhi na kutelekezwa kwa mashamba makubwa, alisema ameziagiza wizara zinazohusika na sekta hizo kukaa chini na kumshauri namna bora ya matumizi ya mashamba hayo ambayo yanaweza kutumiwa na wafugaji na wakulima.

No comments: