MFUMO MPYA WA KUKOKOTOA GHARAMA VYUONI WAKAMILIKA

Mfumo wa Utambuzi wa Gharama za Masomo kwa Kila Mwanafunzi wa Elimu ya Juu , tayari umekamilika na unatarajiwa kuanza kutumika mwaka huu na vyuo vikuu vyote kupanga ada za masomo.
Imeelezwa mfumo huo utatumika kama mwongozo kwa ajili ya Serikali na taasisi za elimu ya juu katika kupanga na kukokotoa gharama za kuendesha programu za masomo na hivyo kupata ada stahili kwa kila programu ya somo.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Ithibati na Uthibiti Ubora wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Savinus Maronga wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mfumo huo.
Maronga alisema matumaini yaliyopo ni kuwa mfumo huo utasaidia kuondoa malalamiko ya muda mrefu ya wadau wa elimu kuhusu gharama na ada za masomo ya elimu ya juu ya hapa nchini.
Alisema mfumo huo umetengenezwa na wataalamu wa hapa nchini kwa kutumia ripoti na matokeo ya ripoti mbalimbali za tafiti za awali na kwa kukusanya taarifa za gharama halisi za ada kwa programu za masomo zinazofundishwa hapa nchini katika vyuo vikuu vya umma na binafsi.

No comments: