NHIF YAONYWA MIKOPO YA DAWA KWA WATOA HUDUMA


Serikali imeuonya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kuwa makini na mpango inaotaka kuuanza katika mwaka ujao wa fedha wa kutoa mikopo ya dawa kwa watoa huduma wote waliosajiliwa.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kebwe Stephen aliyasema hayo Jumanne wiki hii wakati alipotembelea makao makuu ya mfuko huo Kurasini Dar es Salaam na kuzungumza na Menejimenti.
Katika taarifa yake kwa Waziri, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Hamis Mdee alisema katika kukabiliana na uhaba wa dawa, wanatarajia kuanza kutoa mikopo ya dawa kama ilivyo kwa vifaa tiba kwa majaribio, kabla ya kueneza utaratibu huo kwa watoa huduma wote waliosajiliwa.
Lakini Naibu Waziri akautaka Mfuko huo kufanya uangalifu mkubwa katika eneo hilo kwa sababu dawa zimekuwa na gharama kubwa, lakini pia kumekuwapo na watumishi wasio waaminifu wanaoiba dawa.
“Hili la kukopesha dawa ni lazima mliangalie kwa uangalifu mkubwa. Dawa ni eneo lenye gharama kubwa. Kwa mfano, mwaka jana, zimetengwa Shilingi bilioni 80 kwa ajili ya dawa, na sasa zaidi ya asilimia 70 imeshatumika kununulia dawa hizo,” alisema Naibu Waziri.
Dk Kebwe alisema kuwa hali hiyo imefanya upatikanaji wa dawa uwe kwa asilimia 80, lakini akabainisha kuwa hofu yake hiyo ya kuanza kutoa mikopo ya dawa inatokana na ukweli kuwa kuna watumishi wasio waaminifu ambao wamekuwa wakiiba fedha hizo.
“Kuna wizi au udokozi katika eneo hili la dawa. Kwa mfano, kule Magu kuna mfamasia tumemfunga miaka mitano jela kwa wizi wa vitendanishi vya malaria. Tumemfunga huyu kuwa mfano kwa watumishi wengine, na watakaopatikana, sheria itachukua mkondo wake,” alieleza Naibu Waziri.
Alisema hofu nyingine ni kwamba je dawa hizo zitawafikia walengwa, kwani licha ya dawa kuwekwa alama na Serikali kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD), bado kumekuwapo na wizi, kwa watumishi wasio waaminifu wanaoshirikiana na watoa huduma za afya nchini.
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, alisema mbali ya kuanza kutoa mikopo ya dawa kama njia ya kukabiliana na uhaba wa dawa, pia wataongeza ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za uchangiaji na kutoa taarifa ya utekelezaji wa agizo la asilimia 67 ya fedha za uchangiaji zitumike kununulia dawa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF, Balozi Ali Mchumo aliitaka Serikali kuharakisha uundwaji wa bodi maalumu itakayosimamia bei za huduma za afya kama ilivyo kwa simu na maji, akisema itasaidia kupunguza gharama kubwa kwa watoa huduma na bei zisizodhibitiwa.

No comments: