BAGAMOYO WAELEZA WALIVYONUFAIKA MRADI WA KAYA MASKINI


Mtandao wa wabunge katika mashirika ya fedha ya kimataifa  wametembelea wanavijiji wanaonufaika na mradi wa  utoaji fedha kwa kaya masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) wilayani Bagamoyo na kujiridhisha na utekelezaji. 
Wabunge kutoka nchi mbalimbali duniani  wanaunda mtandao pamoja na Benki ya Dunia pamoja na Shirika la Fedha Duniani (IMF) , walitembelea juzi Kijiji cha Kerege na Mlingotini, mkoani Pwani ambako walipata ushuhuda wa walengwa wanavyonufaika. 
Katika kijiji cha Mlingotini, wabunge walitembelea kikundi cha wanawake  cha Mshikamano chenye wanachama 12 kinachoendesha miradi ya ufugaji kuku, mbuzi na uuzaji samaki chini ya mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Tasaf. 
Akizungumza mbele ya ujumbe huo, Mweka Hazina wa kikundi , Stahabu Mrisho alisema Tasaf iliwapatia Sh milioni 13 ambazo walitumia kujenga jengo la biashara, kununua majokofu na pia kwa mtaji.
“Kwa kweli tumenufaika sana na Tasaf. Tumekuwa tukigawana mapato kila mwaka lakini pia akiba na hisa zimetusaidia kuanzisha miradi ya magenge na mama ntilie…Tasaf imetujengea utu na heshima mbele ya jamii,” alisema Stahabu. 
Katika Kijiji cha Kerege, ujumbe huo wa wabunge ulimtembelea mwanakijiji, Jema Lemabi ambaye katika ushuhuda wake, alisema alikuwa na maisha magumu akitegemea kupika na kuuza pombe. 
Kwa mujibu wa Jema, baada ya Tasaf kumwingiza kwenye mpango wa kupewa fedha, alifanya miradi midogo midogo ikiwemo ufugaji wa bata, kuku na kanga na kumudu kujenga nyumba imara iliyoezekwa kwa bati. 
Jema ambaye kwa mujibu wake, alikuwa akiishi nyumba ya makuti, anao bata 49, kuku watatu na kanga wawili. Bei ya bata ni Sh 15,000 na kwamba soko lake kubwa ni Bagamoyo Mjini. 
Mpango huo wa utoaji fedha kwa kaya masikini, umeanza rasmi mwaka huu kutekelezwa nchini kote baada ya majaribio yaliyoanza 2008 mkoani Dodoma na Pwani. Walengwa wake ni watoto na wazee katika kaya masikini zilizo katika mazingira hatarishi. 
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Ladislaus Mwamanga, Mpango huo wa Uhawilishaji Fedha kwa Kaya Masikini chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia, unalenga Watanzania zaidi ya milioni 7.5 katika kaya zipatazo milioni 1.2 wanaoishi katika lindi la umasikini. 
Mtandao wa wabunge wa IMF na Benki ya Dunia unaundwa na wabunge 300 kutoka zaidi ya nchi 140 zinazoendelea na zilizoendelea ambako mashirika hayo ya kimataifa yanafanya kazi. 
Ulianzishwa mwaka 2000. Ziara za wabunge husika nchini ni kujionea shughuli zinazotekelezwa na Benki ya Dunia katika miradi mingine ya maendeleo. 

No comments: