RUBADA WAHIMIZWA KUTIMIZA MALENGO


Wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (Rubada), wamehimizwa kutimiza malengo yote waliyojiwekea katika muda wao wa miaka mitatu kwa kuongeza ufanisi zaidi wa mamlaka hiyo.
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Christopher Chiza alitoa changamoto hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati akizindua bodi hiyo. Alitaka wajumbe wake kufikia malengo waliyojiwekea na kuifanya Rubada kupiga hatua zaidi kimaendeleo.
“Ningependa kuona mnajiwekea malengo yenu na kutimiza kwa wakati ili mtakapomaliza muda wenu, mseme mliletea mafanikio mamlaka hii,” alisema Chiza.
Alisema wizara yake ina imani kubwa  na bodi hiyo ambayo Mwenyekiti wake ni Profesa Lucian Msambichaka, ambaye ni miongoni mwa wachumi waliobobea nchini.
Mbali ya Profesa Msambichaka, wajumbe  wengine katika bodi hiyo ni Profesa Henry Mahoo, Bashir Mrindoko, Gaspar Luanda,  Hosea Mbise, Raphael Dalluti, Dk Ben Moshi, Eline Sikazwe na Nkuvililwa Simkanga.
Alitaka bodi hiyo kuharakisha upatakanaji wa sheria mpya ya mamlaka ili shughuli za uendelezaji Bonde la Rufiji zisikinzane na sheria nyingine.
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Raphael Daluti. 
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Msambichaka aliahidi kuhakikisha maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika yanatekelezwa ili kufikia malengo ya mamlaka.

No comments: