MWENYEKITI PAC ATOA SHUTUMA NZITO UFUTAJI MISAMAHA



Wafanyabiashara wakubwa wanadaiwa kuwatumia baadhi ya wabunge kuhakikisha muswada wa kufuta misamaha ya kodi haupelekwi bungeni.
Tuhuma hizo zilitolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu ya Serikali (PAC), Zitto Kabwe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya  Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh kuwasilisha taarifa yake.
Zitto alisema kuna baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wakishirikiana na wabunge kukwamisha kuletwa kwa muswada huo.
Alisema baadhi ya wabunge hao wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara wakubwa wakiwemo wa makampuni ya uchimbaji wa madini kuwakwamisha.
Kwa mujibu wa Zitto, endapo muswada huo utafika bungeni na kuwekwa kuwa sheria wafanyabiashara hao watafutiwa kodi hivyo wamekuwa wakiogopa.
“Ndugu zangu tusaidieni kuna baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya wabunge kufanya hili,’’ alisema.
Aidha mwenyekiti huyo alisema pia Songas imekuwa ikidaiwa kwa muda mrefu lakini haitaki kulipa deni lake ambalo limekuwa likizidi kuongezeka.
Alisema Songas wamekuwa wakilalamika kuwa nao wanaidai Shirika la Umeme Tanesco.
“Hawa watu wamekopa fedha serikalini zaidi ya bilioni 238 lakini sasa hawataki kurejesha na hizi ni pesa nyingi ni lazima zirudi serikalini,’’ alisisitiza.
Pia Mwenyekiti huyo  alitaka serikali kutumia mashine za kodi, EFDs  katika malipo yake jambo ambalo litasaidia kuokoa fedha nyingi.

No comments: