VIONGOZI WA DINI WAELEZEA UWEZEKANO WA NEEMA YA GESI TANZANIA



Viongozi wa dini kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi, waliopata fursa ya ziara ya kujifunza sekta ya gesi na mafanikio yake nchini Thailand, wamerudi na ushuhuda kwamba  neema ya gesi inawezekana.
Wakizungumza jana asubuhi walipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kutoka katika ziara hiyo ya masomo, viongozi hao walisema mafanikio ya uchumi wa gesi, yatapatikana  ikiwa Watanzania watashirikiana na serikali, kuhakikisha wanafikia uchumi wa gesi asilia.
Katika kushirikiana huko, viongozi hao wamewataka wananchi kuepuka migogoro isiyo na tija huku wakitumia wakati uliopo vizuri kujiandaa na uchumi huo.
Wameeleza kuwa licha ya kuwa gesi itachukua muda mrefu kuanza uzalishaji, ni vema Watanzania wajipe muda bila kuwa waoga kukopa, kujifunza pamoja na kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi pamoja na kujiunga na vyuo vya ufundi.
Makamu wa Askofu wa Kanisa la Anglikana, ambaye ni Askofu wa Kanisa hilo Dayosisi ya Newala, Mtwara, Oscar Mnung’a alisema ni lazima wananchi wakubali kupokea uchumi huo mpya kwa kujifunza, na kujiandaa kukopa ili kuwekeza katika uchumi huo.
“Ili tufikie malengo, tujifunze na tusikubali migogoro isiyo na tija huku tukishirikiana na Serikali kwa kila mmoja kuwa na bidii na juhudi kwani katika nchi hiyo (Thailand), hawana rasilimali kama zilivyo nchini lakini wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa,” alisema Askofu Mnung’a.
Askofu Mnung’a alitaka wananchi washirikiane na Serikali katika kutunga sera zitakazosaidia kuwezesha wageni wakati wa maandalizi, ili washiriki  kusaidia nchi kufikia malengo hayo na baadaye uchumi ushikiliwe na wazawa kama walivyofanya wananchi wa Thailand.
Mhadhiri Mkuu wa Chuo Kikuu cha Stella Maris, Padri Dk Aidan Msafiri, alisema wakiwa nchini humo wamejifunza kuwa kufikia uchumi wa gesi inachukua muda mrefu, na ni lazima gesi isafirishwe kwa kutumia mabomba jambo lililosaidia nchi ya Thailand  asilimia 98 kuwa na nishati ya umeme.
Shekhe wa Mkoa wa Mtwara, Nurdin Mangochi, alisema wananchi wanatakiwa  kuelimishwa na kupata muda wa kujiandaa kwa kutumia vizuri rasilimali watu na ardhi.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mohamed Sinani, alisema jambo kuu lililofanikisha  Thailand kupata neema ya gesi, ni kuwekeza zaidi katika amani pamoja na kupanga mipango ya maendeleo na kuitekeleza.
Alisema baada ya kupata gesi, hawakubweteka bali walipanga mikakati ya kuongeza viwanda na kuzalisha zaidi pamoja na kuendelea na utafiti mbalimbali uliowasaidia kutumia upepo na vyanzo vingine kuzalisha umeme.
Naye Kiongozi wa Serikali katika msafara huo, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, Abdallah Ulega, alisema wanatarajia viongozi wa dini kuwaeleza waumini wao kuwa  gesi duniani kote husafirishwa kwa kutumia mabomba, husaidia kukopa fedha na kushirikisha nchi nyingine katika kupata utaalamu.
Alisema wamejifunza kuwa awali Thailand walitumia wataalamu wa kigeni kutoka Ufilipino na baadaye sera yao ililazimisha wenyeji washirikishwe, baada ya kujifunza utaalamu baada ya kusisitiza kujifunza masomo ya sayansi pamoja na vijana wengi kujiunga na chuo cha ufundi.
Ulega alisema ikiwa hayo yatafanikiwa Tanzania, mafanikio yatapatikana mapema  kuliko ilivyokuwa kwa  Thailand, kwani walianza kuona mafanikio baada ya miaka 40 tangu wagundue gesi, wakati Tanzania ugunduzi wa gesi ulikuwa 2006, lakini mafanikio tayari yameanza kuonekana, ikiwemo matumizi ya magari kwa gesi na mengineyo.

No comments: