KAMATI YAPITISHA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI



Kamati ya Bunge ya Miundombinu, imepitisha Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka ujao wa fedha 2014/2015, ya Sh trilioni 1.2, fedha zilizoelekezwa katika matumizi ya kawaida na ya maendeleo katika wizara hiyo.
Akiwasilisha taarifa ya mapendekezo ya bajeti kwa mwaka ujao wa Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, alifafanua kuwa ili wizara yake iweze kutekeleza majukumu na malengo yake itahitaji kiasi hicho cha Sh trilioni 1.2.
Awali akiwasilisha mapendekezo hayo kwanza, alianza kwa kutoa taarifa ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha unaoishia  2013/14 ambapo wizara hiyo ilitengewa Sh bilioni 381.2 kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
“Hadi kufikia Aprili mwaka huu jumla ya Sh bilioni 372 zilikuwa tayari zimetolewa na Hazina, kiasi hicho ni sawa na asilimia 97.61 ya kiasi kilichokuwa kimepangwa.
Akizungumzia fedha za Mfuko wa Barabara (Road Fund), Magufuli alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha unaoishia mfuko huo  ulipangiwa kukusanya Sh bilioni 504.3 kwa ajili ya wizara hiyo ya ujenzi, Wakala wa Barabara (Tanroads) na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Alisema hadi kufikia Aprili, mwaka huu fedha zote zilizokusanywa zilikuwa zimefikia Sh bilioni 496.2 sawa na asilimia 98.4 ya malengo ya mwaka huo unaoishia wa fedha.
Kamati hiyo ya Bunge baada ya kupitia vipengele vyote ilihitimisha kikao hicho kwa kupitisha mapendekezo ya wizara hiyo ili yaweze kuwasilishwa rasmi katika Mkutano unaoendelea wa Bunge la Bajeti.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba, aliitaka Wizara hiyo ya Ujenzi kuhakikisha inasimamia ipasavyo sheria na taratibu zilizowekwa kwa lengo la kulinda miundombinu mbali mbali inayosimamiwa na wizara hiyo.

No comments: