MWENYEKITI IPP ACHUKIZWA NA TUHUMA ZA CHUKI

Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya IPP Limited, Dk Reginald Mengi amechukizwa na taarifa mbalimbali zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinazomhusisha na tuhuma mbalimbali.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mengi alisema  siku za hivi karibuni kumekuwa na usambazwaji mkubwa wa taarifa hizo ambazo alisema ni za uongo, chuki na uzushi.
Alisema anasikitishwa kuona uzushi huo unachochea na kuifarakanisha jamii kwa misingi ya ukabila, jambo ambalo ni hatari kwa umoja na mshikamano wa Watanzania uliojengeka.
"Mtu yeyote anayediriki kuleta uchochezi wa kikabila hastahili kuwa kiongozi wa ngazi yoyote katika taifa letu," ilieleza taarifa hiyo.
Alisema kuwa yeye ni miongoni mwa Watanzania walio mstari wa mbele kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete katika kusisitiza kuwa rasilimali za asili ni mali ya wananchi na lazima wawe wamiliki wake.
Alisema kulingana na misingi ya Sera ya Taifa ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004, amekuwa akiishawishi serikali kutekeleza sera na sheria za uwezeshaji ili kuwashirikisha Watanzania kikamilifu katika uchumi wa Taifa.
Alisema jitihada zake hizo zimekuwa zikipingwa na kiongozi wa moja za Wizara za Serikali na amekuwa akitumia mbinu na visingizio.
"Mtanzania yeyote hastahili kuwa kwenye uongozi katika ngazi yoyote kwa staili ya kudharau na kuwatukana Watanzania akidhani kwamba kufanya hivyo atajijengea umaarufu," alisema.
Katika taarifa yake hiyo ametaka Watanzania kupuuza uzushi huo unaosambazwa na kwamba wasikubali kuondolewa kwenye hoja ya msingi ya kutaka kujua namna serikali itakavyotekeleza sera na sheria ya uwezeshaji ili kuhakikisha kuwa inawashirikisha katika mchakato mzima wa uchumi wa gesi asilia.

No comments: