WANAFUNZI WAWILI WAUAWA KWENYE UVAMIZI VYUO VIKUU

Matukio matatu ya uvamizi katika makazi ya wanafunzi wa vyuo vikuu kati ya mwaka jana na mwaka juzi, yamesababisha vifo vya wanafunzi wawili nchini.
Aidha, katika matukio hayo, mali mbalimbali kama vile simu, kompyuta mpakato na nguo, viliibwa.
Kutokana na matukio hayo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imeagiza uongozi wa vyuo vya elimu ya juu nchini, kutumia askari polisi wasaidizi au kuanzisha vituo vya  askari kwenye maeneo ya makazi ya wanafunzi na vyuo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima alisema hayo  bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM) aliyetaka kufahamu mpango wa serikali kuhakikisha maeneo  yote ya vyuo vikuu, yanapewa ulinzi wa uhakika baada ya kujitokeza hali ya uvamizi katika makazi na maeneo ya vyuo vikuu.
Pia, mbunge huyo alitaka kufahamu idadi ya wanafunzi walioshambuliwa na mali zilizoharibiwa kutoka kwa wanafunzi hao.
Naibu waziri alisema ulinzi na usalama wa raia, wakiwemo wanafunzi wa shule na vyuo vikuu ni muhimu kwa mustakabali wa elimu ya vijana nchini. Alisema ni jukumu la wote, kama sehemu ya wajibu wa kikatiba na kijamii.
Alisema jeshi la polisi ndicho  chombo chenye dhamana ya kusimamia wajibu huo, litaendelea kuchukua hatua za kupambana na vitendo vya uvamizi na uharibifu mwingine, unaotokea katika vyuo hivyo nchini hususan vya elimu ya juu.
Alisema wanaendelea kushirikiana na mamlaka, hususan uongozi wa vyuo, halmashauri, miji na serikali za mitaa  kuweka miundombinu ya ulinzi shirikishi utakaosaidia kukabili matukio ya uhalifu.
“Aidha, napenda  kuwaasa wanafunzi wa vyuo kutojihusisha na shughuli  na mazingira hatarishi kwa usalama wao na mali zao,” alisema.
Katika swali lake la nyongeza, Mwijage alitaka kufahamu ni mikakati gani ya serikali kuweka vifaa vya usalama katika shule ili kukabiliana na uvamizi katika vyuo hivyo.
Akijibu swali hilo, Silima alisema ulinzi hasa wakati huu wa matishio ya vitendo vya kigaidi ni muhimu katika vyuo vya elimu na sehemu nyingine zenye mikusanyiko katika maeneo muhimu, kama vile hoteli.
Aidha, alisema ni vyema kuweka utaratibu wa kupekua kila anayeingia kuepuka kuingia mtu atakayesababisha madhara.

No comments: