MKURUGENZI MOI AWAASA WENYE KASUMBA YA KUTAKA KUTIBIWA NJE

Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) imeasa Watanzania kuachana na kasumba ya kukimbilia kupata matibabu nje ya nchi kwa magonjwa yanayoweza kutibika  nchini.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na  Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Profesa Lawrence Museru, imesema hakuna haja ya kutumia gharama kubwa kwenda nje wakati huduma inapatikana nchini kwa gharama nafuu.
Taarifa hiyo ililenga kueleza mradi wa jengo jipya la MOI, utakaogharimu zaidi ya Sh bilioni  30  kusaidia  serikali kupunguza gharama za rufaa za kupeleka wagonjwa nje ya nchi kufuata huduma kutokana na  baadhi ya huduma na vipimo kutokuwepo nchini.
Mradi huo utaiwezesha Moi kuwa na vifaa vya kisasa vya Magnetic Resonance Imaging (MRI), CT-SCAN   na Cyberknife Digital Angiography (DSA) ambacho hakipo kabisa Tanzania.
Taasisi hiyo itaweza kuwa na vitanda 20 vya wagonjwa mahututi kutoka vinane vilivyopo sasa, wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu, vitanda 24 ambayo haipo kwa sasa.
Pia kutakuwa na wodi ya wagonjwa wa kuchangia huduma  zikiwa na jumla ya vitanda 240 na wodi za wagonjwa wa kulipia 62 na kuifanya taasisi kuwa na vitanda 380 kutoka 159 vilivyopo na hivyo kuondokana na adha ya wagonjwa kurundikana wodini na kulala kwenye magodoro chini.
Aidha, mradi utatoa fursa ya ajira 243 kwa watanzania katika kada za udaktari, uuguzi, wauguzi wasaidizi na kada nyingine ambazo zimeainishwa kutokana na mahitaji.

No comments: