Waziri wa Uchukuzi, Dk
Harrison Mwakyembe, amesema bajeti ya wizara hiyo ya mwaka 2014/15
iliyopitishwa juzi bungeni, itaifanya reli ianze kukimbia.
Amesema kuwa katika mwaka
wa fedha 2012/13, hali ya reli nchini ilikuwa katika chumba mahututi na
katika mwaka 2013/14, unaomalizika mwezi ujao, reli ilianza kutembea.
Dk Mwakyembe alisema hayo
wakati akifanya majumuisho ya bajeti yake ambayo Bunge, baada ya mjadala mkali,
ilipitishwa bajeti ya Sh bilioni 527.93.
“Mwaka 2012/13 hali ya
reli ilikuwa katika chumba cha mahututi kwa sababu kulikuwa hakuna hela, mwaka
2013/14 reli ilianza kutembea, lakini kwa fedha za sasa reli itaanza kukimbia,”
aliahidi Dk Mwakyembe.
Katika kudhihirisha hali
nzuri, Dk Mwakyembe alisema kufikia Januari mwakani kutakuwa na vichwa vya reli
vipya 51, badala ya vinane vya sasa ikiwa ni idadi kubwa ambayo haijawahi
kutokea nchini.
Alisema kwa kuwa na
vichwa hivyo, uwezo wa reli kubeba mizigo utaongezeka kutoka chini ya tani
200,000 za sasa kufikia tani milioni 1.5 kwa mwaka.
Kuhusu Kampuni ya Ndege
Tanzania (ATCL), alisema tayari Wizara imepeleka katika Baraza la Mawaziri
waraka unaokusudia kuifanya Serikali ibebe deni la Sh bilioni 133 la kampuni
hiyo ili kusafisha mizania na kuifanya kampuni hiyo ipate uwekezaji.
Aidha, Serikali iliahidi
kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza baada ya wabunge
kueleza kuwa hawaridhishwi na utoaji wa fedha, zilizotengwa katika bajeti kwa
ujenzi wa uwanja huo.
Aisisitiza ushiriki wa
sekta binafsi katika miradi mbalimbali ya sekta ya uchukuzi, huku akieleza kuwa
ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam umeongezeka katika kipindi
kifupi.
Katika hatua nyingine,
mjadala mkali ulizuka kuhusu sakata la Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam
(UDA), kiasi cha Dk Mwakyembe kusema suala hilo limeingia katika bajeti yake
wakati kampuni hiyo haiko katika majukumu ya wizara yake.
No comments:
Post a Comment