SABA MBARONI KWA MAUAJI YA POLISI WAWILIWatu saba wamekamatwa na Polisi mkoani Tabora wakituhumiwa kuhusika katika mauaji ya askari Polisi wawili na unyang’anyi wa kutumia silaha,  yaliyofanyika mwezi uliopita. 
Matukio hayo ya unyang’anyi na mauaji yalifanyika Aprili  28, mwaka huu  katika Tarafa ya Usoke Wilaya ya Urambo. 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda alisema askari waliouawa, walikuwa katika harakati za kutekeleza majukumu yao katika eneo hilo la Usoke. Askari hao ni  F.5179 Konstebo Jumanne na G.3388 Konstebo Shaaban.
Kuhusu waliokamatwa, wakituhumiwa kwa mauaji ya askari hao, kamanda aliwataja ni Silvester Mussa maarufu kama Kingwendu (31), mkazi wa Mkuyuni Tambukareli, Mwanza. 
Watuhumiwa wengine ni Sadiki Rushikamwa ambaye anajulikana pia kama Sadiki Milambo au White (28), mkazi wa Mihogoni Tabora na Abel Benedicto maarufu kama Mwendo wa saa (23), ambaye ni mkazi wa Muungano Wilaya ya Urambo.
Wengine waliokamatwa ni Francis Kashinje maarufu Masanja (38) mkazi wa Nansio, Ukerewe, Haji Athanas (50)  mkazi wa Usoke, Mussa Khatibu Ally  (49) ambaye ni mfanyabiashara wa nafaka na mkazi wa Mwanza Road. Mtuhumiwa mwingine ni Ramadhan Mkunya, mkazi wa Tabora. 
Kwa mujibu wa Kamanda, baada ya mahojiano na polisi, watuhumiwa walikiri kushiriki matukio mbalimbali ya unyang’anyi wa kutumia silaha pamoja na mauaji ya askari Polisi wawili.
Alisema baada ya upekuzi, walikutwa na silaha aina ya  Pistol Glock 17, yenye namba za usajili TZ Car 91968, ikiwa na magazini yenye risasi tano.

No comments: