MTUMBWI WAPINDUKA KILOMBERO NA KUUA



Mtu mmoja amekufa na wengine watatu wameokolewa baada ya mtumbwi waliokuwa wakiutumia kupinduka katika Mto Kilombero mkoani Morogoro.
Mtumbwi huo uliokuwa na watu wanne, wawili wakiwa  wavushaji waliokuwa wakivusha shehena ya magunia ya mpunga kutoka upande wa pili wa mto katika Wilaya ya Ulanga.
Ajali hiyo ilitokea juzi saa 12 jioni katika kivuko cha Mto Kilombero ukiwa na watu hao na magunia 11 ya mpunga katika mtumbwi yakisafirishwa  ili kufikishwa mjini Ifakara.
Mmoja wa wavushaji katika mtumbwi huo ambaye amenusurika kifo, Juma Magumbila alisema aliyekufa ni mwenzake anayeshirikiana katika uvushaji, Rajabu Lipindi ‘maarufu kwa jina la Kidilu’.
Alisema siku hiyo walipata kazi za kuvusha magunia 15 ya mpunga kutoka Wilaya ya Ulanga na walipakia katika mtumbwi huo magunia 11  na kuanza safari ya kuvuka Mto  Kilombero.
Hata hivyo alisema wakati wakikaribia kufika upande wa pili, ghafla   dhoruba kali ilitokea na  marehemu aliamua kupiga simu  kuomba msaada, na alipokuwa akiendelea kuwasiliana ndipo mtumbwi  ulipopinduka baada ya kupigwa na wimbi kubwa la maji.
Alisema watu  wawili  waliokuwemo katika mtumbwi wao walikuwa ni wabeba mizigo wa  mpunga ambapo majina yao hakuyafahamu.
Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Francis Miti, ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kilombero  akiwa Mjini Mahenge amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine watatu kuokolewa.
Mkuu wa Mkoa, Joel Bendera akiwa mjini Ifakara, Mei 5, mwaka huu, alifahamishwa kuanzia Februari hadi mwanzoni mwa Mei mwaka huu kuwa watu 11,  walifariki  dunia kwa nyakati tofauti baadhi yao kusombwa na maji na wengine kuliwa na mamba waliotapakaa kando ya m to Kilombero.

No comments: