BENKI YA BOA YASHUSHA RIBA ZA NYUMBABenki ya Afrika (BOA) Tanzania, imetoa ofa ya miezi sita ya pugunzo la riba ya mikopo ya nyumba kutoka asilimia 18 hadi   asilimia 16, ili kuwezesha wananchi wengi kumiliki nyumba.
Meneja Mwandamizi wa Masoko wa benki hiyo, Solomon Haule, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa ofa ya punguzo la riba,  inalenga kuwezesha wananchi kumiliki nyumba.
“Ofa hii imeanza Mei, mwaka huu na itadumu kwa miezi sita,” alisema na kuongeza kuwa  punguzo hilo ni kubwa ikilinganishwa na hali halisi, lakini benki imeamua kufanya hivyo  ili kuwezesha Watanzania wengi kumiliki nyumba za kuishi au biashara kwa kuwa masuala hayo ni ya msingi kwa ustawi wa jamii.
Licha ya punguzo hilo, benki imeongeza muda wa kulipa mkopo kutoka miaka 15 hadi miaka 20 ambayo inatoa fursa kwa watu wengi kuitumia.
Alihamasisha watu wengi hasa vijana kujitokeza na kuitumia fursa hiyo, na kufafanua kuwa anayestahili kupata mkopo ni  mwenye mshahara au kipato cha Sh milioni 1.4 kwa mwezi au watu wawili wanaoshirikiana kutaka kumiliki nyumba kama baba na mama, ambao watakuwa na pato la pamoja la Sh milioni 2 kwa mwezi. 
Akitoa mfano alisema mkopo huo utawawezesha wananchi kununua nyumba za bei rahisi zinazojengwa na mashirika hapa nchini yakiwemo Shirika la Taifa la Nyumba (HNC), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Mafao wa Watumishi wa Umma (PSPF).
“Siyo kwenye mashirika hayo tu, bali hata ukiona nyumba inauzwa na mtu binafsi pia tumia fursa hii kumiliki nyumba,” alisema Solomon.
Akifafanua zaidi alisema ili kupata mkopo huo, mteja atatakiwa kuwa na asilimia 10 na benki itampatia mkopo wa asilimia 90 kwa nyumba mpya na asilimia 20 kwa nyumba iliyotumika.

No comments: