MTIHANI WA HESABU DARASA LA SABA WAMSHINDA PROFESA



Wabunge wamesema hali ya elimu nchini ni mbaya, na kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuunda Tume ya Kudumu ya Elimu, ili kuangalia ubora na kudhibiti sekta hiyo muhimu.
Katika michango yao kwenye mjadala wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi uliotarajiwa kuhitimishwa jana jioni, wabunge wamesema suala la elimu halina siasa, na nchi isipochukua hatua sasa, itakuwa hatari kwa vijazi vijavyo.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alieleza matatizo kadhaa katika mitihani ya Darasa la Saba pamoja na ule wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na kudai kuwa “kuna madudu makubwa.”
Mbatia aliyekuwa ameshika nakala za mitihani hiyo na baadaye kuiwasilisha kwa Naibu Spika, Job Ndugai, alidai baadhi ya mitihani hiyo ni migumu na imewashinda maprofesa wa vyuo vikuu.
“Mimi niliwapatia mitihani hii maprofesa wa vyuo vikuu, imewashinda. Niliwapa huu wa hisabati, akanirudishia akisema mtihani wenyewe haufanyiki.
“Sasa kama yupo mtu humu atamudu kuufanya na kupata alama mia moja, nampa milioni kumi,” alisema Mbatia, huku Naibu Spika akieleza kuwa Waziri Profesa Sospeter Muhongo yuko tayari kuufanya.
“Profesa Muhongo ni profesa wa miamba, kama ataweza huu hapa aje achukue,” alitamba Mbatia.
Mbatia alisema elimu ya Tanzania ni dhaifu na nchi, imeshindwa katika elimu na kuwa suala hilo si la chama cha siasa.
Akitoa majawabu ya hoja zake, Mbatia alimshauri Rais kuunda Tume ya Kudumu ya Elimu ambayo pamoja na mambo mengine, alisema itaangalia ubora na kudhibiti elimu nchini.
Msomi huyo alitaka pia Tume hiyo ifanye kazi ya kuandaa mitaala, kuhariri vitabu akisema Tanzania haina wahariri wa vitabu kama ilivyo kwa vyombo vya habari vyenye wahariri wa aina mbalimbali.
Alizitaja kazi nyingine kuwa ni kufanya utafiti wa kisayansi, kuamua lugha ya kufundishia na kuangalia kwa ujumla tatizo la kushuka kwa elimu.
Alisema elimu siyo bidhaa ya kuuzwa sokoni, bali iwe huduma na kukerwa na kodi nyingi katika elimu na gharama za ada kwa shule binafsi.
“Ni lazima tuukubali ukweli na kukabiliana nao. Elimu yetu imeshuka. Watoto wa walalahoi watapata tabu, kama hatukuisimamia hili, tutapata tabu katika miaka 20 au mia ijayo hasa wakati huu wa sayansi na
teknolojia,” alisema Mbatia.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), aliyesema kuwa elimu iko katika chumba cha wagonjwa wenye uangalizi maalumu (ICU).
Kama Mbatia, Serukamba alishauri kuanzishwa kwa Tume ya kujichunguza kuhusu kuporomoka kwa elimu nchini, akisema “tukubali waseme, tujisahihishe.”
Alisema suala hilo si la mtu mmoja, na kuacha siasa na kuongeza kuwa kama kuna jambo “tunacheza nalo, basi ni elimu, tunaua kizazi kijacho.”
Alisema si vyema kutatua tatizo la elimu kwa kuangalia leo tu, bali uwepo mkakati wa dhati wa muda mrefu, na kutolea mfano Marekani ilivyopitia mfumo wake wa elimu mwaka 1981.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jason Rweikiza (CCM), ambaye anamiliki shule kadhaa nchini, alisema kuna tatizo la shule binafsi kulundikiwa kodi nyingi, na ndio manaa zinatoza ada kubwa.
 “Kuna sijui kodi ya mapato, PAYE, majengo, SDL, yaani ni michango, michango, kodi. Kwa staili hii, ada inapanda, baadaye shule inakufa,” alisema Rweikiza.
Aidha, kama walivyopendekeza wabunge wengine waliochangia jana, mbunge huyo alitaka ukaguzi utiliwe mkazo, akitoa mfano kuwa shule zake hazijakaguliwa tangu mwaka 2005.
Mbunge wa Ngara, Deogratius Ntukamazina (CCM), alisema kwa sasa hakuna Wizara ya Elimu baada ya kuondolewa kwa shule na msingi na sekondari.
Badala yake, akashauri wizara hiyo ibaki kuwa kitovu cha mawazo bora ya elimu kama ilivyo Tume ya Mipango kuhusu masuala ya mipango.
Said Arfi wa Mpanda Mjini (Chadema), licha ya kuzungumzia ukaguzi, alisema bajeti ya elimu imezidi kutegemea wahisani ambao hawatekelezi ahadi zao.
Nyambari Nyangwine wa Tarime (CCM), ambaye ni mtunzi wa vitabu, alipendekeza kuanzishwa kwa Shirika la Uchapaji, kwani vitabu ni moja ya maeneo yanayochangia mporomoko wa elimu nchini.
Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (CUF), alisema mazingira mabovu, ukaguzi kuachwa, shule kukosa maabara na kushuka kwa morali ya walimu, kumechangia kushuka kwa elimu nchini.
Mbunge wa Kilolo, Profesa Peter Msolla (CCM), alitaka masuala ya shule za msingi na sekondari yabaki katika wizara hiyo na irejeshwe wizara ya kusimamia elimu ya juu, huku akisisitiza kuwa upangaji madaraja ni angamizo katika elimu nchini.
Naibu Spika Ndugai naye alipendekeza masuala ya elimu yaondolewe Ofisi ya Waziri Mkuu tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na kurejeshwa kwa wizara hiyo ili yasimamiwe vyema.
Kambi Rasmi ya Upinzani ilisema kuwa malengo na mikakati yote iliyoanishwa ni mizuri, lakini “tunadhani mikakati hiyo imekuwepo muda mrefu, kilichokosekana ni utekelezaji na ufuatiliaji wake.”
Msemaji wake, Susan Lyimo alishauri mikataba ya utendaji kazi katika kila ngazi ya elimu iwekwe wazi ili atakayeshindwa kutekeleza wajibu wake ijulikane atawajibika vipi.

No comments: