MGOMO WA WAFANYAKAZI WA TAZARA UKO PALEPALEWafanyakazi wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara), wamesisitiza msimamo wao wa kuendelea kugoma kutoa huduma, hadi hapo watakapohakikishiwa kwamba malimbikizo ya mishahara yao yatalipwa na malipo ya miezi ijayo, yatafanyika.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (Trawu), Kanda ya Dar es Salaam, Yusuph Mandai, alisema jana Dar e s Salaam kwamba wafanyakazi wa shirika hilo hawatorudisha huduma kama ilivyotarajiwa hadi watakapolipwa madai yao.
Akifafanua zaidi, alisema mshahara wa Februari ambao unatakiwa kulipwa na Serikali ya Tanzania unafikia Sh milioni 140 na mpaka Aprili ni Sh bilioni 1.5.
“Tulipwe kwanza ndio turudishe huduma…na pia ni vyema  tuhakikishiwe mshahara kwa miezi inayokuja,” alisema Mandai mbele ya wafanyakazi hao ambapo pia aliuliaza aliye tayari kurudi kazini anyooshe kidole ambapo hakuona hata mmoja aliyefanya hivyo.
Mandai alipouliza wafanyakazi hao, walio tayari kuendelea na mgomo hadi hapo watakapolipwa waonyooshe vidole kusisitiza suala hilo, wote wakafanya hivyo.
Akizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaban Mwinjaka, alisema fedha kwa ajili ya mishahara ya wafanyakazi hao ziko kwenye mchakato.
“Mimi hapa (Dk. Mwinjaka) ndio natoka Hazina kufuatilia suala hilo…hadi saa sita mchana fedha zilikuwa bado kuingizwa…ila tunafuatilia kwa kina hadi zipatikane,” alisema Dk Mwinjaka.
Juzi akizungumzia suala hilo, Dk Mwinjaka alisema Serikali ya Tanzania imekubali kutoa mshahara wa Aprili na Februari, huku Serikali ya Zambia ikishughulikia mshahara wa Machi na Mei.
Katika hatua nyingine hali za abiria wa usafiri huo zilikuwa za kukatisha tamaa jana ambapo wengi walikuwa wamesambaa bila kujua hatma ya huduma hiyo kwao.
Elizabeth Shaban aliyekuwa akisafiri kwenda Ifakara, Morogoro alisema haelewi utatuzi wa suala hilo kwani wanawasikia viongozi wa wafanyakazi hao wakiwaambia wasafiri endeleeni kusubiria.

No comments: