KAMERA ZA CCTV KUFUNGWA KATIKA MIJI MIKUBWA NCHINI



Serikali imesema iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wa teknolojia ya ufungaji wa vifaa vya ulinzi vijulikanavyo kama CCTV kwa miji mikubwa nchini ikianzia na Jiji la Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe aliliambia Bunge jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM).
Chikawe alisema wizara yake iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo huo ambao kwa kuanzia, utafanyiwa majaribio katika Jiji la Dar es Salaam na kisha kusambazwa miji mingine mikubwa.
“Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Serikali iko katika hatua za mwisho za kuweka vifaa maalumu vya ulinzi katika maeneo mbalimbali ya umma nchini.
“Kwa kuanzia, hivi karibuni tutafunga mfumo huo katika Jiji la Dar es Salaam na kisha kusambazwa katika miji mingine mikubwa kwa kuanzia Zanzibar, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Arusha,” alisema Chikawe.
Alisema utaratibu huo ni wa kawaida sana duniani katika kudhibiti uhalifu na akatolea mfano wa Marekani, ambako kuna msemo kuwa big brother is watching, ukirejea mfumo huo uliowekwa kila mahali.
Katika swali lake la msingi, Lugola alitaka kufahamu kuna sababu gani za msingi kwa Serikali kutofunga vifaa vya kisasa ili kuzuia na kudhibiti uhalifu katika miji mikubwa ya Dar es Salaam, Mwanza, Moshi, Morogoro na Mbeya.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereirra Ame Silima alisema Closed Circuit Television (CCTV) ni muhimu katika kupunguza uhalifu wa aina mbalimbali katika miji nchini.
Alisema kwa kutambua hilo, Jeshi la Polisi katika Programu ya Maboresho inatekeleza jukumu lake la msingi la ulinzi kwa kuwa na miradi 27 ya ICT ukiwemo wa kufuatilia taarifa za usalama barabarani.
“Hata hivyo, ufanisi wa jukumu hili unakwamishwa na ufinyu wa bajeti,” Silima aliliambia Bunge.
Alisema ufungaji wa vifaa hivyo ni jambo mtambuka linaloshirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Wizara ya Ujenzi, Mipango Miji, Serikali za Mitaa na watu binafsi.
“Huu ni mradi mkubwa unaohitaji utafiti wa kutosha wa kimuundo, kisheria na rasilimali fedha. Wizara yangu ni mshauri na msimamizi wa kazi za mradi huu katika kudhibiti uhalifu,” alisema Naibu Waziri.
Alisema Serikali inaendelea kufanya uchambuzi wa mapendekezo ya kibiashara na sekta binafsi ili kuwekeza teknolojia hii na miundombinu yake katika kutimiza malengo ya usalama wa nchi.

No comments: