MKUTANO MKUU WA ALAT WAAHIRISHWA



Mkutano mkuu wa 30 wa kitaifa wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), uliokuwa uanze leo jijini Tanga, umeahirishwa kutokana na kuingiliwa na ratiba za Bunge la Bajeti lililoanza shughuli zake mjini Dodoma jana.
Akitoa taarifa ya mabadiliko ya ratiba ya mkutano huo, kupitia taarifa kwa vyombo vya habari jijini Tanga, Mwenyekiti wa ALAT  Taifa, Dk Didas Massaburi alisema mkutano huo, sasa utafanyika kuanzia  Mei 13, mwaka huu.
Lengo la mabadiliko hayo ni kutoa fursa  kwa baadhi ya wajumbe, wakiwemo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ambao wanawasilisha bajeti zao sasa, kushiriki ipasavyo.
Mkutano huo wa siku nne, unaotarajiwa kufunguliwa na Rais Jakaya Kikwete, awali ulipangwa kufanyika Mei 6 hadi 10 mwaka huu jijini Tanga kwa kushirikisha wajumbe takribani 500.
“Tumewaita hapa ili kuwaeleza wananchi kuhusu mabadiliko ya ratiba ya Mkutano wetu Mkuu ambao tumelazimika kuuahirisha kwa sasa na badala yake utafanyika kuanzia Mei 13 hadi  16, mwaka huu hapa hapa Tanga.”
Dk Massaburi alisema na kuongeza, “Sababu ya kuu ya kufanywa mabadiliko haya ni kama mnavyofahamu kwamba Jumuiya za serikali za mitaa zote ziko chini ya Ofisi ya waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),   sasa kulingana na ratiba ya Bunge la Bajeti wao wataanza kuwasilisha bajeti zao wakati huu (jana).”
“Hivyo isingekuwa jambo rahisi kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pamoja na Waziri wa Tamisemi (Hawa Ghasia) kuacha kuwasilisha bajeti zao ili kuja kuungana nasi mkutanoni wiki hii,” alisema.
Akizungumzia Mkutano Mkuu huo Massaburi ambaye ni  Meya wa Jiji la Dar es Salaam, alisema pamoja na mambo mengine lengo la mkutano huo ni kuadhimisha kwa kutathmini miaka 30 ya mafanikio ya jumuiya ya hiyo tangu kuundwa kwake Desemba 13, 1984.

No comments: