WABUNGE DAR KUSITISHA OPERESHENI SAFISHA JIJI


Umoja wa wabunge  jijini Dar es Salaam,  umesema utasitisha operesheni ya safisha Jiji ambayo inaendelea, na  kuendeshwa kibabe ambapo ni kinyume na makubaliano yao na Mkuu wa Mkoa.
Akitoa kauli hiyo juzi, Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu ambaye pia ni Mwenyekiti wa umoja huo,  alisema operesheni hiyo  imekuwa na matukio ya uvunjifu wa  haki za kibinadamu ikiwemo unyanyasaji wa walemavu.
Alisema watu wenye ulemavu wamekuwa wakishurutishwa kuondoa bidhaa zao kwa nguvu, pamoja na  matukio ya wizi wa bidhaa na fedha za wafanyabiashara hao.
Mbunge huyo alidai kuwa mfumo huo unaoendelea katika operesheni hiyo umekuwa tofauti na makubaliano yao katika kikao cha awali  na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick hivyo inaonekana kuwa amewadharau.
Alisema baada ya kuona utaratibu huo umekwenda kinyume na inavyotakiwa wameamua kuusitisha na kuupanga tena hivyo watatoa tamko rasmi ili utaratibu huo uwe kwa maslahi ya wananchi na kwa Taifa kwa ujumla.
Opereshini hiyo ya safisha jiji ilianzishwa na Halmashauri ya Jiji kusudi kuweka jiji kuwa safi, wakati huo mgambo wa jiji na wahusika wengine wa operesheni hiyo walionekana kutumia nguvu kuwaondoa wafanyabiashara hao,  hata kutumia silaha kuwasambaratisha.


No comments: