KITABU CHA KERO ZA MUUNGANO CHAANDALIWAWakati Muungano ukiwa hoja kuu katika mchakato wa Katiba mpya uliofikia katika ngazi ya mjadala wa Bunge Maalumu, Serikali imeandaa kitabu maalumu kinachoelezea historia, utekelezaji wa mambo ya Muungano, mafanikio, changamoto, fursa na matarajio ya Muungano kwa miaka ijayo.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema hayo jana alipokuwa akiwasilisha Makadirio ya Bajeti ya Ofisi yake ya Sh bilioni  105.5 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo ya ofisi yake.
Kwa mujibu wa Pinda, kitabu hicho kitatumika kama rejea kwa kizazi chetu na vizazi vijavyo, ili kuendelea kulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliodumu kwa miaka 50 sasa.
“Tutaendelea kuulinda Muungano wetu kwa nguvu zote tukiwa na uelewa kwamba, katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Watanzania wameishi kwa amani na kufanya kazi zao za kujiletea maendeleo wakiwa upande wowote wa Muungano,” alisema Pinda.
Akitetea hoja yake ya kulinda Muungano, Pinda alisema takwimu zinaweka jambo moja wazi kwa Muungano  kwamba zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania  wote, wamezaliwa baada ya Muungano. 
“Sasa tuliozaliwa kabla ya Muungano ni chini ya asilimia kumi.  Kwa mujibu wa takwimu hizo, Tanzania nzima ina watu 44,926,923.  Kati yao, watu 40,640,425, sawa na Asilimia 90.6 ni wa umri wa siku moja hadi miaka 50.
“Takwimu hizo zina maana kwamba, asilimia 90.6 ya watu wote wamezaliwa ndani ya Muungano na nchi wanayoifahamu ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Sote tunawajibika kuwatendea haki watu hawa kwa kuulinda, kuuimarisha na kuudumisha Muungano wetu,” alisema Pinda.
Hata hivyo kwa mujibu wa Pinda, takwimu hizo za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, zimebainisha jambo lingine kwamba asilimia 7.7 ya Watanzania ambao ni watoto, ni yatima.
“Hali ya utegemezi nchini ni kubwa kutokana na ukweli kuwa kati ya Watanzania milioni 44.9, asilimia 50.1 ni watoto wenye umri chini ya miaka 18. Aidha, takwimu zimebainisha kuwa asilimia 7.7 ya Watanzania ni watoto yatima.
“Kutokana na hali hiyo, ni jukumu letu kama Taifa kuweka mipango madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo katika sekta za huduma za jamii, ili hatimaye kila mwenye uwezo wa kufanya kazi achangie ipasavyo katika kukuza uchumi na maendeleo ya nchi yetu,” alisema.
Pinda alisema pato la Taifa katika mwaka 2013, lilikua kwa asilimia 7  ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.9 mwaka 2012 na  ongezeko hilo limetokana na ukuaji mzuri wa shughuli za huduma za mawasiliano, viwanda, ujenzi na huduma za fedha.
Hata hivyo, alifafanua kuwa pamoja na uchumi  kukua kwa kasi ya asilimia 7.0 kwa mwaka 2013 na pato la Mtanzania kuongezeka, kiwango hicho siyo kikubwa kiasi cha kuwezesha umaskini wa wananchi kupungua kwa kasi.
“Utafiti wa kitaalamu unaonesha kwamba, ili umaskini upungue kwa kasi kubwa, uchumi unatakiwa kukua kwa zaidi ya asilimia nane kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo.  Ukuaji huo pia unatakiwa kulenga sekta ambazo zinagusa maisha ya watu wengi, hususan kilimo, mifugo na uvuvi,” alisema Pinda.
Katika kuinua sekta ya kilimo, Pinda alisema Serikali kupitia Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa, inategemea kuvutia uwekezaji na kuanzisha kilimo cha mashamba makubwa 25 ya kilimo cha kibiashara kwa mazao ya mpunga na miwa kwa utaratibu wa kuwaunganisha wakulima wakubwa na wadogo wanaozunguka mashamba hayo.
“Serikali imeendelea kushirikisha Washirika wa Maendeleo kuchangia Programu ya Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
“Miongoni mwa malengo ya Programu hiyo ni kuwaunganisha wakulima wadogo na mnyororo wa thamani wa kibiashara wa  kampuni  kubwa za ndani na nje ya nchi. Ili kufikia lengo hilo, Serikali imeanzisha Mfuko Chochezi wa Uendelezaji wa Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania,” alisema Pinda.
Alifafanua kwamba mfuko huo utatoa mitaji itakayogharamia hatua za awali za miradi inayotoa tija ya haraka, ambayo imebainishwa kwenye Mpango Mkakati wa Uwekezaji.
Vilevile alisema Mfuko huo utahamasisha biashara inayolenga kumuinua mkulima mdogo kwa kumuunganisha na mnyororo wa thamani na kampuni kubwa.
Mbali na makadirio ya bajeti kwa ajili ya Ofisi yake, Pinda pia aliomba Bunge limuidhinishie Sh  bilioni 479. 22 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo ya Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na taasisi zake.
Ofisi za wakuu wa mikoa ziliombewa Sh bilioni  267. 90, halmashauri zote zimeombewa Sh trilioni 4.23 na Bunge Sh bilioni  132.6 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo.

No comments: