MKAGUZI MKUU, TAKUKURU WAITWA SAKATA LA IPTL


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) pamoja na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wameagizwa kuchunguza na  kujiridhisha kama kweli upo uchotaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Escrow iliyokuwa imefunguliwa ndani ya Benki Kuu (BoT)  kwa ajili ya kampuni ya  Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema hayo jana bungeni mjini hapa wakati akihitimisha mjadala wa wabunge kuhusu bajeti ya mwaka wa fedha 2014/15 ya ofisi yake ambayo jana wabunge walipitisha bajeti hiyo ya Sh trilioni tano. 
Alisema baada ya tuhuma hizo kuanza kujitokeza, aliamua kumwuliza CAG ni namna gani wafanye kuhusu masuala hayo. “CAG akaniambia alipoona kwenye magazeti akaamua kuyafanyia kazi,” alisema.
Kwa mujibu wa Pinda, CAG alizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Gavana wa Benki Kuu, Benno Ndulu, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felschemi Mramba ili kupata picha ya yaliyojiri katika mchakato mzima.
Alisema Katibu Mkuu, Nishati na Madini pia alimwandikia barua kumwomba CAG  afanye uchunguzi wa kina ili tuhuma hizo zilizotolewa  kwenye  vyombo vya habari, zipatiwe ufumbuzi.
“Maelezo niliyoyapata, kamati ya PAC ilipokuwa imemwita Katibu Mkuu kuhusu jambo hilo, alitoa maelezo kwamba ameshamwelekeza CAG kufanya uchunguzi kuhusu jambo hilo. PAC nayo ilimwandikia CAG afanye uchunguzi.
“Na mimi nimemwambia CAG fanya uchunguzi wako halafu tuletee serikalini tuletee bungeni…kwa tuhuma zenyewe zilivyo, itabidi tuwahusishe na Takukuru nao ili nao watusaidie kupata ukweli juu ya jambo hili. Kwa sababu kwa maelezo na mtiririko ulivyo ni tuhuma zinazojitokeza ambavyo vyombo hivi vinao uwezo kubaini kipi cha ukweli na kipi si cha kweli,” alisema na kuomba Bunge likubali CAG akamilishe kazi hiyo.
Pinda alisema uamuzi wa kuingiza takribani Sh bilioni 20 katika akaunti ya Escrow haukuwa wa kificho kwa kuwa fedha hizo zilikuwa za IPTL na ndivyo mahakama ilivyokuwa imeelekeza.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, suala la IPTL ni la muda mrefu tangu 1994. Wakati huo serikali baada ya kuona lipo tatizo la umeme, ilitafuta mtu aliyekuwa tayari kuzalisha umeme.
Mkataba ulionesha umeme utakaozalishwa utauzwa Tanesco na ulikuwa na sehemu mbili kwa maana ya malipo ya uwepo wa mtambo na pia uzalishaji.
Wakati wakiendelea, ulitokea mgogoro upande wa Tanesco na IPTL kuhusu kodi  inayopaswa kulipwa na baadaye ukazaa kesi iliyobidi ipelekwe mahakama ya kimataifa ya usuluhishi.
Wakati mgogoro huo ukiendelea, Serikali ilibidi ifungue akaunti ya Escrow na fedha kutoka Tanesco zikawa zikilipwa kwenye akaunti hiyo.
Fedha zilizokuwa zimewekwa kwenye akaunti hiyo ni za IPTL na katika uamuzi wa mahakama ikaamriwa fedha hizo zipelekwe IPTL kwa kuwa ni fedha zao. Kukawa na mvutano. “Fedha hizo zikapelekwa IPTL, jambo tunalopaswa kama wabunge kujiridhisha nalo ni je, VAT ipo kweli au haipo?,” alisema Pinda.
Alisema baada ya kesi kumalizika, Tanesco na IPTL walikaa wakatazama kiasi kinachodaiwa, wakafika mahali wakakubaliana ni kiasi gani cha fedha kilipwe. Alisema kwa upande huo, kama kuna masuala yanaweza kupatiwa majibu bila mjadala na kuvutana. 
“Kubwa ni pale zogo limejikita zaidi kwenye kuondoa fedha kutoka akaunti ya Escrow kutoka Benki Kuu kupeleka IPTL na maswali ambayo yamejitokeza kwamba kodi haikulipwa, ufisadi upo, unajiuliza wa nini kama fedha ile ilikuwa ni fedha yao,” alihoji Pinda.
Ufafanuzi huo wa Waziri Mkuu ulitokana na kauli iliyotolewa juzi na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR Mageuzi) akituhumu baadhi ya viongozi na watendaji serikali kuchota fedha hizo katika akaunti hiyo.
Mbunge huyo alitawataja Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema kwamba walihusika.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luhaga Mpina amepinga kauli iliyotolewa na Kafulila bungeni juzi akisema Gavana wa BoT aliiambia kamati hiyo kuwa alilazimika kuruhusu fedha zitolewe kutokana na shinikizo la vigogo wa serikali.
Mpina ambaye aliomba mwongozo wa spika jana, alikanusha Gavana huyo wa Benki Kuu kuiambia kamati yake maneno hayo.
“Nilidhani mimi ndiye sikusikia maneno hayo; lakini nilipowasiliana na wenzangu kwenye kamati, walisema suala hilo halikusemwa,” alisema Mpina.
Aliendelea kusema, “Watu wengine wanaweza kusema kwa sababu mimi ni mwana CCM kwa hiyo ninapendelea, lakini kuna wabunge watano kwenye kamati kutoka upinzani waliosema Gavana wa BoT hakusema hivyo.”
Mpina alisema kamati yake ilimwandikia gavana wa benki kuu kufika kwenye kamati yao kuhusu suala hilo la fedha za akaunti ya Escrow.
Alisema, “Baada ya Kafulila kuzungumza hilo, niliwaita wajumbe wangu, tukaulizana, kila mmoja alisema si kweli kilichosemwa. Kila kitu ninacho hapa tena kwa maandishi, nitawasilisha kwako mheshimiwa Spika.”
Wakati baadhi ya wabunge jana walishinikiza Waziri Mkuu aunde tume ya bunge kuchunguza suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG), Jaji Werema alisema fedha hizo haziko mikononi mwake.
“Mnapomuuliza Waziri Mkuu akubali kuundwa kwa kamati, kwa mujibu wa kanuni hiyo siyo kazi yake. Huo ni wajibu wa spika ndivyo inavyosemekana. Lakini wazo na hapa lazima kama kuna mafisadi, na Werema anatajwa ni miongoni, lazima ijulikane. Wala hakuna kufunika vitu vyote viko wazi na mimi ninavyo vya wazi vingi kabisa…na uamuzi uliofanyika, uchunguzi ufanywe na CAG ni sawa sawa,” alisema.
Wakati huo huo Spika wa Bunge, Anne Makinda, ameonya wabunge dhidi ya kutumiwa na watu wengine wa nje ya Bunge kwa manufaa yao.
Makinda alisema baadhi ya wabunge wamekuwa wakija bungeni wakiwa wamebeba hoja za watu binafsi na kuzitetea.
Katika kile alichosema vitendo hivyo vinaweza kuhatarisha uhai wa bunge, alisema hata kama mbunge ameambiwa jambo nje ya Bunge, ni lazima kulipima kabla ya kulileta bungeni.
“Sasa nimeanza kuona kuna baadhi yetu wanakuja na hoja zao kutoka nje na kuzileta humu kuzitetea,” alisema na kusisitiza kuwa kitendo hicho si sahihi na kinaharibu heshima ya bunge.
Ingawa alisema ushawishi ni suala la kawaida, lakini alisema mbunge anapopata mawazo ya mtu mwingine, anapaswa kuchanganya na ya kwake na si kuingiza hoja hiyo moja kwa moja bungeni.

No comments: