WANAFUNZI 237 WATIMULIWA CHUO CHA POLISI KWA VYETI FEKI


Jeshi la Polisi nchini limewatimua jumla ya wanafunzi wa uaskari 237 wa Chuo cha Taalumu ya Polisi Moshi, kutokana na makosa mbalimbali yakiwemo ya kughushi vyeti, matatizo ya kiafya pamoja na makosa ya kinidhamu.
Akitoa taarifa hizo jana katika ukumbi wa chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi, Kamishna wa Utawala na Utumishi ndani ya Jeshi la Polisi, Thobias Andengenye alisema wanafunzi wa uaskari waliofukuzwa kwa kughushi vyeti ni 212 na wengine 25 ni kwa makosa ya kinidhamu na matatizo ya kiafya.
Andengenye alisema katika kuhakikisha jeshi la polisi linaendelea kuwa na askari wenye weledi na uaminifu kwa raia na taifa, lilianzisha uhakiki wa vyeti kwa kushirikiano na Baraza la Mitihani Taifa, ambapo wanafunzi wa uaskari 212 walionekana vyeti vyao ni vya kughushi.
"Kutokana na maboresho ya jeshi la polisi la kutaka askari wenye weledi na kulitumikia taifa, tumeona tuanze uhakiki wa vyeti, kwa kushirikiana na baraza la mitihani, ambapo vyeti vya wanafunzi wa uaskari 212 kati ya walioripoti vimeonekana ni vya kughushi, hivyo tumeona tuwaachishe masomo," alisema CP Andengenye.
Alisema tatizo kama hilo linaweza kusababisha taifa kupata madhara makubwa kwa kuwa na watu ambao sio wataalamu husika, hivyo jeshi la polisi litaendelea kufanya uchunguzi kwa kushirikiana na taasisi nyingine kwa lengo la kuzuia mianya hiyo.
Alibainisha wanafunzi waliofukuzwa wamefunguliwa mafaili yao, kwa ajili ya kuwafuatilia mienendo yao wakiwa uraiani na kutokana na mafunzo ambayo wamekwisha yapata, ili wasije kujihusisha na masuala ya uhalifu.
Andengenye alisema wanafunzi wote walibainika kughushi vyeti watachukuliwa hatua mara baada ya upelelezi kukamilika kwa kushirikiana na taasisi nyingine, ikiwemo Baraza la Mitihani la Taifa.
Alisema jeshi la polisi lina mkakati wa kubadilisha mfumo wa ajira, ambapo watakuwa wanapokea wanafunzi kutoka vyuoni na mashuleni, ambapo wataachana na njia ya kupokea maombi kwa njia ya barua hali itakayosaidia kupata watu wanaopenda kazi za uaskari.
Pia jeshi hilo linaenda kwenye maboresho ya alama za vidole nchi nzima, ambapo patakuwepo na data za watu wote waliofanya makosa, hivyo endapo mtu yeyote atakapofanya kosa na kukimbilia sehemu nyingine, atakapokamatwa kosa lingine taarifa zake zitasoma makosa yake yote.
Andengenye alisema kitendo chochote cha kughushi ni kosa la jinai, ambapo aliwataka wananchi wote kuacha tabia kama hizo na badala yake wafuate taratibu na sheria zilizopo kwa ustawi wa taifa.

No comments: