MISINGI YA UTAWALA BORA YAENDELEA KUWEKWA



Serikali ya Tanzania imeendelea kuweka misingi imara ya kufanyia kazi maoni ya wananchi kuhusu hali ya utawala bora nchini, kama yalivyobainishwa kupitia Ripoti ya Hali ya Utawala Bora iliyoandaliwa na Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).
Tanzania ni miongoni mwa nchi 34, kati ya 54, za AU zilizokwishajiunga na Mpango wa APRM. Tanzania ilijiunga na mchakato huu mwaka 2004 na Bunge liridhia Februari 1, 2005.
Taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana na APRM Tawi la Tanzania, ilieleza kuwa tayari wizara mbalimbali zilizoguswa na ripoti hiyo, zimekwishakuelekezwa kufanyia kazi changamoto zilizobainishwa na kutoa taarifa.
“Baada ya Rais Jakaya Kikwete kuiwasilisha Ripoti ya Tanzania mbele ya wakuu wenza wa nchi za APRM mwaka jana, Serikali ilitakiwa kuanza kufanyiakazi changamoto za kiutawala bora zilizobainishwa.
“Utekelezaji huo unaendelea vyema. Masuala mengi ya kikatiba yameingizwa kwenye rasimu inayojadiliwa. Masuala ya kisera na kitaasisi tayari yamefikishwa katika taasisi husika kwa ajili ya kufanyiwakazi,” ilisema taarifa hiyo.
APRM ni nyenzo mojawapo ya kutathmini mafanikio na changamoto za utekelezaji wa shughuli za maendeleo na ujenzi wa utawala bora barani Afrika, ikiwemo Tanzania katika ili kutafakari kwa pamoja namna bora zaidi ya kuziendeleza juhudi hizo.
Kuhusu mchakato wa sasa wa Katiba unaoendelea, taarifa hiyo ilisisitiza: “Tumeaswa kuutumia vyema mchakato wa sasa wa Mabadiliko ya Katiba kuijenga Tanzania bora zaidi katika miaka mingine mingi ijayo.”

No comments: