BAJETI YA WIZARA YA KILIMO NA USHIRIKA YAPITA



Pamoja na wabunge kuchachamalia makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa kuondoa shilingi mara kadhaa, bajeti hiyo ilipita pamoja na maboresho.
Maboresho hayo ni pamoja na Serikali kupitia Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Christopher Chiza, kuitisha mkutano wa wadau wa kilimo cha pamba mapema wiki hii na kufanya mchanganuo wa baadhi ya matumizi ambayo hayakufafanuliwa vizuri  kwa ajili ya mafunzo kwa wakulima.
Pamoja na mvutano mkali,Bunge limeidhinisha Bajeti ya Sh bilioni 318 .7 kwa ajili ya matumizi ya Wizara hiyo.
Katika hatua nyingine, juhudi za Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) kutaka kukwamisha bajeti hiyo, ziligonga mwamba baada ya wabunge wa CCM, kukataa kumunga mkono na hivyo kungwa mkono na wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi.
Mbunge huyo alidai Chiza ameshindwa kusimamia watendaji wake, kiasi cha kuachia kuingizwa kwa mbegu na mbolea feki na kusababisha wakulima kupata hasara.
“Wabunge wa CCM simameni, mniunge mkono niondoe Shilingi,“ alisema mbunge huyo huku akiwa amesimama ingawa hakuna mbunge wa CCM aliyesimama, huku baadhi ya wabunge wakapaza sauti na kusema Mbunge wa Sikonge, Saidi Mkumba (CCM) ameunga mkono hoja na wabunge wa upinzani wakimwambia Lugola “hamia huku”.
Hata hivyo, Mkumba aliposimama alisema  hawezi kumuunga mkono Lugola kwa sababu katika kujenga hoja yake, anataka kugombanisha wajumbe.
“Siwezi kumuunga mkono  kabisa Lugola kwa sababu katika hoja yake anataka kugombanisha wajumbe na wapiga kura wetu. Lugola hawezi kuwa msemaji wa wabunge, suala la kutaka waziri ajiuzulu si jepesi, ajipime kwanza utendaji wake na kama amemaliza ahadi zote alizowahaidi wananchi wa jimbo lake,” alisema Mkumba.
Hata hivyo. Lugola alisema lengo la hoja yake ni kuzungumzia wakulima na hajagombanisha wabunge na wapiga kura wao.

No comments: