EXIM BANK YATOA MAGODORO 60 HOSPITALI YA MWANANYAMALA


Benki ya Exim ya Tanzania imeadhimisha Sikukuu ya Mama Duniani kwa kuchangia magodoro 60 katika wodi ya wazazi ya Hospitali ya Mwananyamala  jijini Dar es Salaam. 
Imefanya hivyo ili kutoa heshima kwa kinamama wote na kuunga mkono jitihada za kuboresha afya ya uzazi nchini.  
Kwa sasa, Hospitali ya Mwananyamala ambayo ni hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dar es Salaam,  inatoa huduma kwa kinamama wanaotarajia kujifungua zaidi ya 3,100 kwa mwezi, ikiwa na vitanda 136 tu katika wodi hiyo ya wazazi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi magodoro hayo hospitali hapo mwishoni mwa wiki, Meneja Msaidizi Masoko wa benki hiyo, Anita Goshashy alisema mchango huo ni moja ya utekelezaji wa shughuli za benki, zinazolenga kuisaidia jamii inayoizunguka. 
“Mwaka jana, Benki ya Exim imeweza kufikia faida ya shilingi bilioni 20 na tumekuwa na utamaduni wa kurejesha kile tukipatacho kutoka kwa jamii. Sasa, leo hii tuko hapa Mwananyamala kukabidhi vitu hivi, ikiwa kama njia ya kutambua mchango wa mama zetu na kuonyesha jinsi gani tunaisaidia jamii inayotuzunguka kama benki,” alisema  Goshashy. Aliongeza kuwa benki itaendelea kuipiga jeki jamii, hususani katika sekta za afya, mazingira na elimu. 
Goshashy alisisitiza kuwa, “Leo hii tunakabidhi magodoro haya ili kuweza kusaidia kuboresha uzazi ulio salama. Kina mama wengi wanaotarajia kujifungua hufariki wakati wakijifungua. Mchango wetu leo utasaidia katika katika kuboresha hali hiyo hapa hospitalini Mwananyamala. Jitihada zetu hazitaishia hapa. Tutaendelea kufanya kazi karibu na jamii inayotuzunguka.” 
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk Sophinias Ngonyani aliipongeza Benki ya Exim kwa msaada huo. Aliongeza kuwa msaada umewafikia kwa wakati muafaka. Alitaka taasisi nyingine za kifedha na makampuni mengine nchini, kuiga mfano huo. 
“Kwa niaba ya Jamii ya Hospitali ya Mwananyamala, ningependa kuelezea shukrani zangu za dhati kwa hatua nzuri mliyoichukua, kuweza kutusaidia vitanda hivi ambavyo vitatumika kwa kinamama, ambao tunawathamini kwa kiasi kikubwa maishani mwetu. Mchango huu utasaidia jamii ya Mwananyamala kwa kiasi kikubwa  sana,” alisema Dk Ngonyani.

No comments: