UTEKELEZAJI MATOKEO MAKUBWA TPA WAENDELEA VIZURI TPAUtekelezaji wa mkakati wa Matokeo Makubwa Sasa katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), umeelezwa kwenda vizuri.
Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na TPA ya kati ya Julai 2013 na Machi 2014 kuhusu utekelezaji wa mkakati huo, imeonesha pamekuwa na maendeleo makubwa na kuongezeka kwa ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam, ikilinganishwa na kabla ya Julai mwaka jana.
Pamoja na mambo mengine, mkakati wa Matokeo Makubwa Sasa unalenga kubadilisha bandari za Tanzania na hasa ile ya Dar es Salaam kuwa kitovu kikuu cha uchumi Tanzania na kutoa ushindani katika ukanda wa Afrika.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, pamekuwa na ongezeko la mizigo katika bandari hiyo kwa muda huo unaofikia tani milioni 10.95, ikiwa ni mafanikio kwa asilimia 84.2 kabla ya kufikia lengo la tani milioni 13 kwa   mwaka 2013/2014.
Muda wa meli kukaa bandarini kwa mwezi Machi mwaka huu, ilikuwa siku 6.1 kwa meli, mafanikio ya asilimia 82.0 kabla ya kufikia lengo la siku 5 kwa meli.  
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, muda wa kukaa kwa mizigo bandarini kutoka nje kwa Machi mwaka huu, ilikuwa siku 10.0 kwa kontena, ikilinganishwa na lengo la siku 7 kwa kontena.
“Hali hii imesababishwa na miundombinu mibovu ya reli na kutegemea usafirishaji kwa njia ya barabara kwa kiwango kikubwa,” imeeleza ripoti hiyo.
Uwezo wa kutoa magari bandarini, umeongezeka kwa asilimia 100.7 kwa mwezi Machi mwaka huu, na magari 604 yakitolewa kwa awamu.
Ripoti hiyo ilisema kuwa kwa Machi 2014,  lengo la kutumia siku tatu kwa lori moja la mizigo kuwa limeondoka bandarini, limefikiwa kwa asilimia 81.1, kwani sasa lori moja linatumia siku 3.3. 

Kwa sasa kwa mujibu wa ripoti hiyo, juhudi za kufanya bandari hiyo kufanya kazi kwa saa 24 kwa siku saba za wiki, ziko katika hatua za mwisho. 

Ripoti ya makubaliano ya wadau wote wa Serikali na sekta binafsi, iliyofikiwa Februari mwaka huu, itajadiliwa hivi karibuni tayari kwa utekelezaji. 

Ikizungumzia mfumo wa Kituo Kimoja cha Huduma za Bandari,   unaolenga kurahisisha kazi za nyaraka bandarini hapo, ripoti hiyo inasema tayari mfumo huo umeshaanza kutumika tangu  Aprili 25, mwaka huu.

No comments: