MISHAHARA YAPANDA, 'PAYE' KUPUNGUA HADI TARAKIMU MOJA


Rais Jakaya Kikwete, amewaahidi wafanyakazi nchini kuwa katika mwaka ujao wa fedha ambao Mpango wa Bajeti umeonesha kuwa itakuwa ya Sh trilioni 19.7, Serikali itapandisha mishahara ya wafanyakazi.
Pia ameonya taasisi za umma na waajiri wote wanaokwepa kuanzisha mabaraza ya kazi na matawi ya vyama vya wafanyakazi katika maeneo yao ya ajira, kuwa kitendo hicho ni kinyume cha Sheria na kuiagiza Wizara ya Kazi na Ajira, kufuatilia suala hilo, na kuwachukulia hatua watakaobainika.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema suala hilo la mishahara ni kilio cha wafanyakazi cha siku nyingi, lakini pamoja na uhaba wa fedha unaoikabili Serikali, imekuwa ikijitahidi kila mwaka, kuongeza mishahara hiyo kulingana na uwezo wake.
 “Najua hiki ndio kilio chenu na wote mnasubiria kwa hamu Serikali inasema nini? Nawaahidi kuwa katika hotuba ya Bajeti Waziri wa Kazi na Ajira, itabainisha wazi, kiwango cha mshahara ambacho Serikali imekiongeza katika mishahara ya wafanyakazi,” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo, alisema Serikali haitoweza kupandisha mishahara hiyo na kufikia ombi la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA),  kwamba mishahara ya kima cha chini ipande kutoka Sh 240,000 za sasa na kufikia Sh 750,000, kwa kuwa bado pato la Serikali liko chini haliwezi kumudu kiasi chote hicho.
“Kwa sasa pekee Serikali inatumia asilimia 44 ya Bajeti yake na asilimia 10 ya Pato la Taifa kulipa mishahara ya wafanyakazi, kiwango ambacho ni kikubwa, lakini kwa kuwa ina dhamira ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi wake, imekuwa ikilipa fedha hizo,” alisisitiza.
Alisema Serikali kwa muda mrefu imekuwa ikijali wafanyakazi hasa Serikali ya Awamu ya Nne, ambapo mwaka 2005 kima cha chini cha mishahara ya wafanyakazi kilikuwa Sh 65,000, lakini baada ya kuona ulazima wa kupandishwa kimepanda na kufikia Sh 240,000 ambayo nayo itaongezwa hivi karibuni.
Pamoja na hayo, Rais Kikwete alionesha kutoridhishwa na namna sehemu kubwa ya sekta binafsi, isivyozingatia viwango vya mishahara vinavyopangwa na Serikali, hali inayochangia kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara baina ya waajiri na waajiriwa.
“Hili ni tatizo, lakini pia kuna malalamiko mengi tunayapokea  serikalini kutoka kwa wafanyakazi wa sekta binafsi ambayo kwa kweli yanatuumiza, sina budi kukutana na waajiri ili tuzungumze kiundani na kutafuta ufumbuzi,” alisema Rais Kikwete.
Akizungumzia suala la Kodi ya Mapato (P.A.Y.E), Rais Kikwete, alisema ombi hilo nalo kama ilivyo nyongeza ya mishahara ni la muda mrefu, na kuwaahidi wafanyakazi hao kuwa nalo linafanyiwa kazi ili kupunguza kutoka asilimia 13 inayotozwa kwa sasa na kufikia tarakimu moja.
Katika jitihada za kupunguza matatizo ya wafanyakazi,   Rais Kikwete alisema Serikali ina mpango wa kuanzisha Mfuko Maalumu wa Fidia kwa wanaokumbwa na matatizo wakiwa kazini, kutokana na ukweli kuwa kwa sasa wafanyakazi wengi wanaumia na kupoteza maisha katika ajira zao bila fidia yoyote.
Alisema kupitia mpango huo, Serikali itachangia katika mfuko huo kila mwaka asilimia moja ya mishahara yote, na kwa kuanzia katika mwaka ujao wa fedha tayari zimetengwa Sh milioni 40 kwa ajili ya mfuko huo, huku waajiri wakitakiwa kuchangia asilimia 0.5 katika mfuko huo kila mwaka.
Kuhusu suala la baadhi ya waajiri na taasisi kukwepa kuanzisha mabaraza ya kazi na matawi ya vyama vya wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi, Rais Kikwete alisema Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini pamoja na Sheria ya Utumishi wa Umma, zimebainisha wazi umuhimu kila sehemu ya kazi kuwa na mabaraza na matawi hayo.
Alisema kazi ya mabaraza na matawi hayo, ni kusimamia maslahi na kutetea haki za wafanyakazi, lakini pia yanatumika kama daraja la mawasiliano baina ya wafanyakazi na Serikali na  kukwepa kuanzisha au kuanzisha na kutofanya vikao ni kosa kisheria.
“Hawa wanaokwepa kuanzisha matawi na mabaraza haya watawanyima haki wafanyakazi wao, lakini pia Serikali tunajua kuwa wapo waajiri wameanzisha mifumo yao iliyo kinyume na Sheria za nchi kwa kukwepa kuanzisha matawi haya, Wizara ya Kazi na Ajira tumeni wakaguzi wenu na kuwafichua waajiri hawa,” aliagiza.
Katika hatua nyingine Rais Kikwete, aliitaka Wizara ya Kazi na Ajira kutoa kipaumbele kifedha na kutenga mfuko maalum kwa ajili ya kuwezesha Baraza la Usulushi kutekeleza wajibu wake, kwa kuwa kwa sasa Baraza hilo, linashindwa kuwajibika ipasavyo kutokana na uhaba huo wa fedha.
Rais Kikwete pia alisisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa mfumo wa utatu, ambao ni wafanyakazi, waajiri na Serikali katika kutatua matatizo ya wafanyakazi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa utawala bora.
“Kaulimbiu ya mwaka huu ya maadhimisho haya imebainisha wazi kuwa Utawala bora, utumike kutatua kero za wafanyakazi, ni kweli kabisa, migogoro mingi ya wafanyakazi inatokana na kukiukwa na kutotekelezwa kwa kanuni za utawala bora, hili sote linatuhusu waajiri, wafanyakazi na Serikali,” alisema.
Aliwahakikishia Watanzania kuwa Serikali inajitahidi kuhakikisha uchumi wa nchi unakua na kugusa maisha ya watu, ambapo tayari katika tatizo la mfumuko wa bei, imejitahidi na sasa hali imetengemaa.
Naye Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, alimpongeza Rais Kikwete kwa kupatiwa tuzo ya utawala bora Afrika, na kuwataka waajiri nchini kutumia fursa hiyo kumuenzi kiongozi huyo kwa kuhakikisha wanafuata nyayo na kusimamia utawala bora, ili kupunguza migogoro ya kazi.
Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya, akiwasilisha risala ya wafanyakazi katika maadhimisho hayo, aliiomba Serikali ishughulikie matatizo yanayowakabili wafanyakazi ya uboreshaji wa mishahara, kupunguzwa kwa kodi ya P.A.Y.E na kuboreshewa pensheni.
“Utafiti wetu wa mwaka 2006 ulibaini kiwango cha chini cha mshahara kilichostaafu ni Sh 350,000…utafiti wa mwaka 2013 ulibaini kiwango cha mshahara kuwa Sh 750,000 kwa mwezi kwa sababu ya kushuka kwa thamani ya Shilingi pamoja na mfumuko wa bei, tunaomba utusaidie haya yatekelezwe sasa,” alisisitiza.

No comments: