KATIBA IKISHINDIKANA SASA ITASUBIRI MIAKA IJAYO


Viongozi wa kitaifa wameonya kuhusu muelekeo wa mchakato wa kupata Katiba mpya, kwamba usiachiwe kuvuruga amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, huku Rais Jakaya Kikwete akihadharisha kuwa isipopatikana, Katiba hiyo, itatafutwa tena miaka ijayo.
Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, akikabidhi nyumba 30 za watumishi wa afya wa Mkoa wa Singida, zilizojengwa kwa ufadhili wa  Global Fund Round 9 na kusimamiwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa juzi, aliwataka Watanzania kuhakikisha mchakato wa Katiba mpya unaoendelea hivi sasa, hauvurugi amani, upendo na utulivu uliopo nchini.
Kwa upande wake Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, akihutubia katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani  Mei Mosi jana Bwawani Zanzibar, alisema zipo dalili kuwa baadhi ya wanasiasa wameanza kuutumia mchakato wa Katiba mpya vibaya, kwa kuanza kujenga uhasama wa kisiasa ambao hatma yake ni nchi kuingia katika machafuko. 
Mkapa alisema amani na utulivu uliopo nchini kwa miaka mingi havina budi kudumishwa na kukuzwa, ili kuenzi waasisi wa Taifa letu.
 “Vyovyote utakapoishia mchakato huu wa Katiba…amani, upendo na utulivu lazima vihimili maisha yetu,” alisema Mkapa na kuongeza: “Tuhitilafianeni lakini bila kupigana.” 
Dk Shein kwa upande wake kutokana na dalili alizozibaini, amewatahadharisha wananchi na wanasiasa, kwamba mchakato wa kupata Katiba mpya usiwe chanzo cha kuvuruga amani na utulivu uliopo na kujenga uhasama.
 Alisema kwa muda mrefu sasa Zanzibar imekuwa ikipata mafanikio makubwa, ikiwemo kuimarika kwa amani na utulivu ambao umewafanya wananchi kuishi vizuri kwa maelewano na kuzika tofauti za itikadi za kisiasa.
Alifafanua kwamba mchakato wa Katiba kupitia Bunge Maalumu la Katiba, unatokana na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba  na hakuna sababu za kujenga chuki na uhasama kama inavyoanza kujitokeza.
“Wananchi wa Zanzibar nawaasa kwamba Bunge Maalumu la Katiba lipo kwa mujibu wa Sheria na wananchi kamwe wasijenge chuki na uhasama utakaosababisha nchi yetu kurudi katika siasa za chuki na uhasama,” alisema.
Rais Kikwete akizungumza katika Sikukuu ya Wafanyakazi Dar es Salaam jana, aliwataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, kutumia ipasavyo nyongeza ya siku 60 watakayopatiwa kwa kuja na uamuzi wenye manufaa kwa Watanzania, vinginevyo ikishindikana, Katiba hiyo, itatafutwa tena miaka ijayo. 
“Mimi Rais kazi yangu nimemaliza ya kuteua wajumbe, sasa yanayoendelea mle ndani ni ya kwao…kwa kweli nasikitishwa na kilichokuwa kikijiri ndani ya Bunge lile na kuniacha na maswali kuwa hivi tusi ni hoja?” alihoji Kikwete.
Alisema kuteuliwa kwa wajumbe hao kutoka taasisi, itikadi na maeneo tofauti, ilikuwa ni moja ya mbinu ya kuibua mijadala mbalimbali ambayo ingewezesha kupatikana kwa Katiba nzuri yenye manufaa kwa Watanzania. 
“Hata wazungu wanasema acha mawazo 100 yagongane ili kupatikane wazo moja la msingi, lakini naamini kuwa wajumbe hawa hawataishia pale, watakaa na kutumia likizo waliyonayo na kuja na mawazo mazuri na kutuletea Katiba mpya,” alisisitiza.
Aliwataka Watanzania kuwatumia wajumbe wanaowawakilisha katika Bunge hilo, kuwasilisha mawazo yao badala ya kuwaachia watoe mawazo yao jambo ambalo ni rahisi kwao kutekwa na mawazo ya wengine. 
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, Nicholaus Mgaya, alisema shirikisho hilo, limesikitishwa na mwenendo wa Bunge hilo la Katiba, ambao umesababisha wananchi kupoteza imani nalo na kushauri wajumbe wote waliohusika na makosa yaliyojitokeza kujirekebisha katika Bunge lijalo. 
Tangu kuanza kwa mchakato huo baada ya Rasimu ya Katiba mpya kukabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete, na wakati wote wa  awamu ya kwanza ya Bunge Maalumu la Katiba, mjadala mkubwa ulihamia katika muundo wa Muungano.
Rasimu hiyo imependekeza muundo wa Muungano kuwa wa serikali tatu; Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano. 
Hata hivyo, hoja mbalimbali zimekuwa zikitolewa kupinga muundo wa serikali tatu kutokana na kuhusishwa na uvunjifu wa amani, upendo na mshikamano wa Watanzania, ambao umedumishwa kwa miaka 50 ya Muungano sasa chini ya muundo wa serikali mbili.
Baadhi ya hoja hizo zilitolewa na Profesa Bonaventura Rutinwa wa Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambaye amekuwa akieleza namna muundo wa Muungano wa serikali tatu utakavyoharibu mshikamano, umoja na upendo wa Watanzania.
Alisema kitendo cha Katiba ya Zanzibar kuita eneo hilo la Tanzania kuwa ni nchi na kutoa haki kwa Wazanzibari, ambazo hazitatolewa kwa wasio Wazanzibari, kitaharibu umoja na mshikamano uliopo, kama Tanganyika ikianzishwa katika mfumo unaopendekezwa wa serikali tatu. 
“Sasa kwa kuwa Zanzibar tayari ina Katiba yake, inayotoa na kulinda haki za kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa Wazanzibari, huhitaji nguvu za kinabii kubashiri kuwa Katiba ya Tanganyika ikija, itatoa na kulinda haki za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa Watanganyika.
“Hii ikitokea, itasababisha wananchi kutoka Tanganyika wanaoishi Zanzibar na Wazanzibari wanaoishi Tanganyika kushindwa kudai haki zao za uraia kisheria,” alionya Profesa Rutinwa.
Alihitimisha kuwa katika mazingira hayo, mfumo unaopendekezwa wa serikali tatu, utafifisha mshikamano wa Watanzania na serikali za nchi washirika, na katika hali mbaya zaidi utazalisha kero mpya za Muungano zitakazokuwa na nguvu ya kuvunja Muungano.

No comments: