MGOGORO MORAVIAN BADO MOTO, WENGINE WASALI CHINI YA MTI

Mgogoro wa Kanisa la Moravian Jimbo la Misheni Mashariki, Dar es Salaam umeendelea kusababisha vurugu za kiimani baada ya waumini wa kanisa hilo Ushirika wa Kinondoni kugawanyika, wengine wakisalia chini ya mti na baadhi kanisani.
Pande zote mbili za mgogoro huo uliodumu kwa miaka miwili sasa, umeliambia mwandishi unataka amani, lakini mazungumzo kati yao yamekuwa yakigonga mwamba hadi uongozi wa dunia (Unity Board) wa kanisa hilo, ukaingilia kati.
Sababu za mgogoro huo zinadaiwa kuwa ni ukiukwaji wa Katiba na ubadhilifu wa fedha za kanisa zaidi ya Sh milioni 500 unaodaiwa kufanywa na Mwenyekiti wa Jimbo, Mchungaji Clemence Fumbo. Hata hivyo uongozi wa dunia uliamuru Fumbo aendelee na uongozi na kuagiza ukaguzi wa hesabu ufanywe, jambo ambalo upande unaompinga, umegoma.
Kutokana na mgogoro huo ambao sasa unashughulikiwa na uongozi wa dunia wa kanisa hilo unaosisitiza amani kupitia mazungumzo ya pamoja kwa pande zote mbili, vurugu zimekuwa zikiibuka katika ushirika za kanisa hilo mara kwa mara.
Jana, mwandishi alishuhudia baadhi ya waumini wakisali nje ya Kanisa la Kinondoni na wengine wakiwa kanisani na viongozi wa pande zote mbili walipozungumza na mwandishi, walisisitiza kutaka amani lakini wakasema inakwamishwa na vitendo vya vurugu vya mara kwa mara makanisani.
“Kuna kikundi cha watu 20 kinaongoza vurugu katika kanisa, vyombo vya usalama vinashindwa kusimamia haki kwa kuwa watu wanatumia nguvu ya fedha, tunachotaka sisi ni amani na kurejea kusali kanisani.
“Katika kipindi cha mgogoro hakuna mwenye haki, mpaka Jumapili ijayo lazima turejee kanisani,” alisema Katibu wa Mawasiliano wa Jimbo hilo, mchungaji Emmaus Mwamakula alizungumza katika ibada ya chini ya mti jana. Ibada hiyo ya chini ya mti ilikuwa na watu wengi ambao walidai ndio wajenzi wa jengo la kanisa.
Mzee Kiongozi wa Baraza la Ushirika huo, Erasto Kasekwa akiwa na wazee wenzake katika Ibada hiyo ya chini ya mti, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, walikuwa wakisalia ukumbini na wenzao kanisani, lakini alhamisi walifungiwa mlango na mnyororo wasiingie kusali.
“Polisi walifika na wazee 13 walienda polisi kutoa maelezo lakini wakaja watu wenye fedha wa upande mwingine wakabadilisha maelezo ikaonekana sisi tuna hatia, tupo hapa nje kuepusha vurugu kwa kuwa tungeweza kulazimisha kuingia kwa kuwa sisi ndio tumejenga kanisa lakini hatutaki, Mungu ndie mtetezi wetu, tunachotaka ni amani,” alisema Kasekwa.
Akizungumza kwa niaba ya waliosalia kanisani, Makamu Mwenyekiti wa Jimbo hilo, Mchungaji Sauli Kajula anayempinga Mchungaji Fumbo, alisema waumini wanaosalia nje walifanya fujo na kuvunja baadhi ya milango ya ofisi na nyumba ya mchungaji na sasa wanasubiri uamuzi wa kiaskofu kuhusu tukio hilo.
Mchungaji wa Ushirika huo, James Mwakalile alisema vurugu kanisani hapo zilianza Februari 23 na kuzidi Mei 22, baada ya upande mwingine kupinga utekelezaji wa Sinodi inayodaiwa kufanyika Oktoba 2012 na ya Desemba 2013.
Mikutano (Sinodi) hiyo haikushirikisha pande zote na Unity Board ilieleza si rasmi na lazima kutafutwa suluhu kabla ya mikutano hiyo.  
Majirani wa eneo hilo, waliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, wamechoshwa na vurugu hizo kwani zinatia doa imani ya Kikristo ambayo kwa asili ni ya amani na kuwataka wakae kumaliza tofauti zao badala ya kuliabisha jina la Yesu.

No comments: