USAFIRI WA TRENI DAR WATENGEWA SHILINGI BILIONI 2.92

Wakati abiria wa treni inayotoa usafiri katika Jiji la Dar es Salaam wakifikia milioni 1.4, Serikali imetenga Sh bilioni 2.92 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa njia mpya za reli jijini humo kutokana na huduma hiyo kukua na kupendwa na wananchi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) ilisafirisha abiria 1,343,763 katika mwaka 2013 ikilinganishwa na abiria 230,009 waliosafirishwa katika mwaka 2012 kutoka Stesheni hadi Ubungo Maziwa.
Aidha, kwa upande wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), alisema abiria 1,460,506 walisafirishwa katika mwaka 2013 ikilinganishwa na abiria 148,524 waliosafirishwa katika mwaka 2012 kutoka Mwakanga hadi Kurasini. Usafiri huo ni maarufu kwa jina la Treni ya Mwakyembe.
Akiwasilisha bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2014/15 bungeni Dodoma juzi usiku, Dk Mwakyembe alisema wizara inaendelea na mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma hiyo, ukiwamo mpango wa kuvutia sekta binafsi kuwekeza kwenye usafiri wa treni Jijini.
“Katika mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali imetenga Shilingi bilioni 2.92 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa njia mpya za reli Jijini Dar es Salaam zikiwemo zile za kwenda maeneo ya Pugu, Mbagala/Chamazi, Luguruni/Kibaha na Bunju/Kerege.
“Na ujenzi wa mchepuo wa njia ya reli kutoka Ilala block post hadi Stesheni ili kuepusha mwingiliano wa treni ya abiria kutoka Stesheni kwenda Ubungo na ile ya mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam,” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema katika hotuba yake ya 2013/14, alitoa taarifa ya Wizara kuunda Kamati maalumu chini ya uenyekiti wa Naibu Waziri wa Uchukuzi kwa ajili ya kuchambua, kuainisha, na kushauri mipango na mikakati ya kuboresha usafiri wa abiria jijini Dar es Salaam; kazi ambayo imekamilishwa katika kipindi cha Julai, 2013 hadi Aprili, 2014.
“Mikakati iliyoainishwa inahusu kuongeza eneo la ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa usafiri jijini kutoka umbali wa kilometa 20 za sasa hadi kilometa 50 ili kujumuisha wilaya za Kibaha, Kisarawe, Mkuranga na Bagamoyo.
“Aidha, wazabuni tisa wamejitokeza kufanya upembuzi yakinifu wa kupanua huduma za treni ya abiria kwenda maeneo ya Kibaha, Bunju, Mbagala na Pugu, sita kati yao, wamewasilisha maandiko kuhusu ya kina kuhusu mradi huo,” alieleza Dk Mwakyembe.
Alisema uchambuzi wa maandiko yao unaendelea ili kumpata Mtaalamu Mwelekezi mmoja ndani ya mwaka huu wa fedha, na kwamba kuhusu uwekezaji katika usafiri huo wa treni jijini Dar es Salaam kwa utaratibu wa PPP, kampuni kadhaa za ndani na nje ya nchi zimeonesha ari ya dhati.
“Serikali imewafungulia milango na kuwasubiri wapige hatua ya kwanza. Wizara kwa kushirikiana na TRL na RAHCO imeamua kuanzisha kampuni tanzu ya kutoa huduma za usafiri wa reli mijini ambayo itatoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki,” alisema Waziri wa Uchukuzi ambaye anaomba Bunge limuidhinishie Sh 527,933,790,000.

No comments: